Zaburi 4
Sala ya jioni ya kuomba msaada
Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Daudi.
1 Nijibu nikuitapo,
Ee Mungu wangu mwenye haki!
Nipumzishe katika shida zangu;
nirehemu, usikie ombi langu.
2 Enyi watu, mtabadilisha utukufu wangu
kuwa aibu hadi lini?
Mtapenda udanganyifu
na kufuata miungu ya uongo hadi lini?
3 Fahamuni hakika kwamba Mwenyezi Mungu amewatenga
wale wamchao kwa ajili yake;
Mwenyezi Mungu atanisikia nimwitapo.
4 Katika hasira yako, usitende dhambi.
Tulieni kimya mkiwa vitandani mwenu,
mkiichunguza mioyo yenu.
5 Toeni dhabihu zilizo haki;
mtegemeeni Mwenyezi Mungu.
6 Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye
kutuonesha jema lolote?”
Ee Mwenyezi Mungu, tuangazie nuru ya uso wako.
7 Wewe umejaza moyo wangu kwa furaha kubwa
kuliko watu waliopata nafaka na divai kwa wingi.
8 Nitajilaza chini na kulala kwa amani,
kwa kuwa wewe peke yako, Ee Mwenyezi Mungu,
waniwezesha kukaa kwa salama.