Zaburi 6
Sala ya kuomba msaada wakati wa taabu
Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Mtindo wa sheminithi.*Sheminithi ni mtajo mmojawapo katika lugha ya uimbaji. Zaburi ya Daudi.
1 Ee Mwenyezi Mungu, usinikemee katika hasira yako,
wala usiniadhibu katika ghadhabu yako.
2 Unirehemu Mwenyezi Mungu,
kwa maana nimedhoofika;
Ee Mwenyezi Mungu, uniponye,
kwa maana mifupa yangu
ina maumivu makali.
3 Nafsi yangu ina uchungu mwingi.
Hadi lini, Ee Mwenyezi Mungu, hadi lini?
4 Geuka, Ee Mwenyezi Mungu, unikomboe,
uniokoe kwa sababu ya fadhili zako.
5 Hakuna mtu anayekukumbuka
akiwa amekufa.
Ni nani awezaye kukusifu
6 Nimechakaa kwa kulia kwa huzuni;
usiku kucha natiririsha
kitanda changu kwa machozi;
nimelowesha kiti changu
kwa machozi yangu.
7 Macho yangu yamedhoofika kwa kuhuzunika,
yamedhoofika kwa sababu ya adui zangu wote.
8 Kaeni mbali nami, ninyi nyote mtendao mabaya,
kwa maana Mwenyezi Mungu amesikia kulia kwangu.
9 Mwenyezi Mungu amesikia kilio changu kwa huruma,
Mwenyezi Mungu amekubali sala yangu.
10 Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika,
watarudi nyuma na waaibishwe kwa ghafula.
*^ Sheminithi ni mtajo mmojawapo katika lugha ya uimbaji.
†Zaburi 6:5 Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, yaani Shimo lisilo na mwisho.