Zaburi 50
Ibada ya kweli
Zaburi ya Asafu.
Mwenye Nguvu, Mungu, Mwenyezi Mungu,
asema na kuiita dunia,
tangu mawio ya jua
hadi mahali pake liendapo kutua.
Kutoka Sayuni, penye uzuri mkamilifu,
Mungu anaangaza.
Mungu wetu anakuja na hatakaa kimya,
moto uteketezao unamtangulia,
akiwa amezungukwa na tufani kali.
Anaziita mbingu zilizo juu,
na nchi, ili aweze kuwahukumu watu wake:
“Nikusanyieni watu wangu waliowekwa wakfu,
waliofanya agano nami kwa dhabihu.”
Nazo mbingu zinatangaza haki yake,
kwa maana Mungu mwenyewe ni hakimu.
 
“Sikieni, enyi watu wangu, nami nitasema,
ee Israeli, nami nitashuhudia dhidi yenu:
Mimi ndimi Mungu, Mungu wenu.
Sikukemei kwa sababu ya dhabihu zako,
au sadaka zako za kuteketezwa,
ambazo daima ziko mbele zangu.
Sina haja na fahali wa banda lako,
au mbuzi wa zizi lako.
10 Kwa maana kila mnyama wa msituni ni wangu,
na pia makundi ya mifugo juu ya vilima elfu.
11 Ninamjua kila ndege mlimani,
nao viumbe wa kondeni ni wangu.
12 Kama ningekuwa na njaa, nisingewaambia ninyi,
kwa maana ulimwengu ni wangu,
na vyote vilivyomo.
13 Je, mimi hula nyama ya mafahali
au kunywa damu ya mbuzi?
14 Toa sadaka za shukrani kwa Mungu,
timiza nadhiri zako kwake Yeye Aliye Juu Sana,
15 na uniite siku ya taabu;
nami nitakuokoa, nawe utanitukuza.”
16 Lakini kwake mtu mwovu, Mungu asema:
“Una haki gani kunena sheria zangu
au kuchukua agano langu mdomoni mwako?
17 Unachukia mafundisho yangu
na kuyatupilia mbali maneno yangu.
18 Unapomwona mwizi, unaungana naye,
unapiga kura yako pamoja na wazinzi.
19 Unakitumia kinywa chako kunena maovu,
na kuuongoza ulimi wako kwa hila.
20 Unamsengenya ndugu yako bila kukoma,
na kumsingizia mwana wa mama yako.
21 Mambo haya unayafanya, nami nimekaa kimya,
ukadhani Mimi ni kama wewe kabisa.
Lakini nitakukemea
na kuweka mashtaka mbele yako.
 
22 “Yatafakarini haya, ninyi mnaomsahau Mungu,
ama sivyo nitawararua vipande vipande,
wala hapatakuwa na yeyote wa kuwaokoa:
23 Atoaye dhabihu za shukrani ananiheshimu mimi,
naye aiandaa njia yake
ili nimwoneshe wokovu wa Mungu.”