Zaburi 57
Kuomba msaada
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu”. Utenzi wa Daudi. Baada ya kumponyoka Sauli pangoni.
Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,
kwa maana nafsi yangu inakukimbilia.
Chini ya uvuli wa mabawa yako nitakimbilia
hadi maafa yapite.
 
Namlilia Mungu Aliye Juu Sana,
Mungu anayetimiza makusudi yake kwangu.
Hutumana msaada kutoka mbinguni na kuniokoa,
akiwakemea wale wanaonifuatilia vikali;
Mungu huutuma upendo wake na uaminifu wake.
 
Niko katikati ya simba;
nimelala katikati ya wanyama wenye njaa kali,
watu ambao meno yao ni mikuki na mishale,
ambao ndimi zao ni panga kali.
 
Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
utukufu wako na uenee duniani kote.
 
Waliitegea miguu yangu nyavu,
nikachoshwa na dhiki.
Wamechimba shimo katika njia yangu,
lakini wametumbukia humo wao wenyewe.
 
Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti,
moyo wangu ni thabiti;
nitaimba na kusifu kwa nyimbo.
Amka, nafsi yangu!
Amka, kinubi na zeze!
Nitayaamsha mapambazuko.
 
Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kati ya mataifa;
nitaimba habari zako, kati ya jamaa za watu.
10 Kwa maana upendo wako ni mkuu, waenea hadi mbinguni,
uaminifu wako unazifikia anga.
 
11 Ee Mungu, utukuzwe juu mbinguni,
utukufu wako na uwe duniani pote.