Zaburi 59
Kuomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu”. Utenzi wa Daudi. Sauli alipotuma wapelelezi nyumbani mwa Daudi ili wamuue.
Ee Mungu, uniokoe na adui zangu,
unilinde kutokana na hao wanaoinuka dhidi yangu.
Uniponye na watu watendao maovu,
uniokoe kutokana na wanaomwaga damu.
 
Tazama wanavyonivizia!
Watu wakali wananifanyia hila,
ingawa Ee Mwenyezi Mungu, mimi sijakosea
wala kutenda dhambi.
Sijatenda kosa; hata hivyo wako tayari kunishambulia.
Inuka unisaidie, uone hali yangu mbaya!
Ee Mungu, Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,
uliye Mungu wa Israeli,
zinduka uyaadhibu mataifa yote;
usioneshe huruma kwa wasaliti waovu.
 
Hurudi wakati wa jioni,
wakibweka kama mbwa,
wakiuzurura mji.
Tazama yale wanayotema kutoka vinywa vyao,
hutema panga kutoka midomo yao,
nao husema, “Ni nani atakayetusikia?”
Lakini wewe, Mwenyezi Mungu, uwacheke;
unayadharau mataifa hayo yote.
 
Ee nguvu yangu, ninakutazama wewe,
wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,
10 Mungu wangu unayenipenda.
 
Mungu atanitangulia,
naye atanifanya niwachekelee
wale wanaonisingizia.
11 Lakini usiwaue, Ee Bwana, ngao yetu,
au sivyo watu wangu watasahau.
Katika uwezo wako wafanye watangetange
na uwashushe chini.
12 Kwa ajili ya dhambi za vinywa vyao,
kwa ajili ya maneno ya midomo yao,
waache wanaswe katika kiburi chao.
Kwa ajili ya laana na uongo wanaotamka,
13 wateketeze katika ghadhabu,
wateketeze hadi wasiwepo tena.
Ndipo itakapofahamika katika miisho ya dunia
kwamba Mungu anatawala katika Yakobo.
 
14 Hurudi jioni,
wakibweka kama mbwa,
wakiuzurura mji.
15 Wanatangatanga wakitafuta chakula,
wasipotosheka hubweka kama mbwa.
16 Lakini mimi nitaziimba nguvu zako,
asubuhi nitaimba kuhusu upendo wako;
kwa maana wewe ndiwe ngome yangu
na kimbilio langu wakati wa shida.
17 Ee uliye Nguvu zangu, ninakuimbia sifa.
Wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,
Mungu unayenipenda.