Zaburi 70
Kuomba msaada
(Zaburi 40:13-17)
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Maombi.
Ee Mungu, ufanye haraka kuniokoa;
Ee Mwenyezi Mungu, njoo hima unisaidie.
Wale wanaotafuta kuniua,
waaibishwe na kufadhaishwa;
wote wanaotamani kuangamizwa kwangu,
warudishwe nyuma kwa aibu.
Wale wanaoniambia, “Aha! Aha!”
na warudi nyuma kwa sababu ya aibu yao.
Lakini wote wanaokutafuta
washangilie na kukufurahia,
wale wanaoupenda wokovu wako siku zote waseme,
“Mwenyezi Mungu ni mkuu!”
 
Lakini mimi bado ni maskini na mhitaji;
Ee Mungu, unijie haraka.
Wewe ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu;
Ee Mwenyezi Mungu, usikawie.