Zaburi 79
Maombi kwa ajili ya wokovu wa taifa 
 Zaburi ya Asafu. 
  1 Ee Mungu, mataifa yameuvamia urithi wako,  
wamelinajisi Hekalu lako takatifu,  
wameifanya Yerusalemu kuwa magofu.   
 2 Wametoa maiti za watumishi  
kuwa chakula cha ndege wa angani  
na nyama ya watakatifu wako  
kwa wanyama wa nchi.   
 3 Wamemwaga damu kama maji  
kuzunguka Yerusalemu yote,  
wala hakuna yeyote wa kuwazika.   
 4 Tumekuwa kitu cha aibu kwa majirani zetu,  
cha dharau na mzaha kwa wale wanaotuzunguka.   
 5 Hata lini, Ee Mwenyezi Mungu? Je, wewe utakasirika milele?  
Wivu wako utawaka kama moto hadi lini?   
 6 Mwaga ghadhabu yako kwa mataifa yasiyokukubali,  
juu ya falme za hao wasioliitia jina lako,   
 7 kwa maana wamemrarua Yakobo  
na kuharibu nchi ya makao yake.   
 8 Usituhesabie dhambi za baba zetu,  
huruma yako na itujie hima,  
kwa maana tu wahitaji mno.   
 9 Ee Mungu Mwokozi wetu, utusaidie,  
kwa ajili ya utukufu wa jina lako;  
tuokoe na kutusamehe dhambi zetu  
kwa ajili ya jina lako.   
 10 Kwa nini mataifa waseme,  
“Yuko wapi Mungu wenu?”  
Mbele ya macho yetu,  
dhihirisha kati ya mataifa  
kwamba unalipiza kisasi damu iliyomwagwa  
ya watumishi wako.   
 11 Kilio cha huzuni cha wafungwa kifike mbele zako;  
kwa nguvu za mkono wako  
hifadhi wale waliohukumiwa kufa.   
 12 Walipize majirani zetu mara saba  
aibu walizovurumisha kwako, Ee Bwana.   
 13 Ndipo sisi watu wako, kondoo wa malisho yako,  
tutakusifu milele;  
tutasimulia sifa zako  
kizazi hadi kizazi.