Zaburi 84
Kuionea shauku nyumba ya Mwenyezi Mungu
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya wana wa Kora.
Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,
makao yako yapendeza kama nini!
Nafsi yangu inatamani sana,
naam, hata kuona shauku,
kwa ajili ya nyua za Mwenyezi Mungu;
moyo wangu na mwili wangu
vinamlilia Mungu Aliye Hai.
 
Hata shomoro amejipatia makao,
mbayuwayu amejipatia kiota
mahali awezapo kuweka makinda yake:
mahali karibu na madhabahu yako,
Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,
Mfalme wangu na Mungu wangu.
Heri wale wanaokaa nyumbani mwako,
wanaokusifu wewe daima.
 
Heri wale ambao nguvu zao ziko kwako,
na njia ziendazo Sayuni zimo mioyoni mwao.
Wanapopita katika Bonde la Baka*maana yake Bonde la Vilio,
hulifanya mahali pa chemchemi,
pia mvua za vuli hulijaza kwa madimbwiau baraka.
Huendelea toka nguvu hadi nguvu,
hadi kila mmoja afikapo
mbele za Mungu huko Sayuni.
 
Ee Bwana Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni,
sikia maombi yangu;
nisikilize, Ee Mungu wa Yakobo.
Ee Mungu, uitazame ngao yetu,
mtazame kwa wema mpakwa mafuta wako.
 
10 Siku moja katika nyua zako ni bora
kuliko siku elfu mahali pengine;
afadhali ningekuwa bawabu katika nyumba ya Mungu wangu
kuliko kukaa katika mahema ya waovu.
11 Kwa kuwa Bwana Mwenyezi Mungu ni jua na ngao;
Mwenyezi Mungu hutoa wema na heshima;
hakuna kitu chema anachowanyima
wale ambao hawana hatia.
 
12 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,
heri mtu anayekutumaini wewe.

*Zaburi 84:6 maana yake Bonde la Vilio

Zaburi 84:6 au baraka