Zaburi 103
Upendo wa Mwenyezi Mungu
Zaburi ya Daudi.
1 Ee nafsi yangu, umhimidi Mwenyezi Mungu.
Vyote vilivyo ndani yangu
vilihimidi jina lake takatifu.
2 Ee nafsi yangu, umhimidi Mwenyezi Mungu,
wala usisahau wema wake wote:
3 akusamehe dhambi zako zote,
akuponya magonjwa yako yote,
4 aukomboa uhai wako na kaburi,
akuvika taji la upendo na huruma,
5 atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema,
ili ujana wako uhuishwe kama wa tai.
6 Mwenyezi Mungu hutenda haki,
naye huwapa hukumu ya haki
wote wanaodhulumiwa.
7 Alimjulisha Musa njia zake,
na watu wa Israeli matendo yake.
8 Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mwenye neema;
si mwepesi wa hasira, bali amejaa upendo.
9 Yeye hatalaumu siku zote,
wala haweki hasira yake milele,
10 yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu
wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu.
11 Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia,
ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha;
12 kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi.
13 Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake,
ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowahurumia wale wanaomcha;
14 kwa kuwa anajua tulivyoumbwa,
anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.
15 Kuhusu mwanadamu, siku zake ni kama majani,
anachanua kama ua la kondeni;
16 upepo huvuma juu yake nalo hutoweka,
mahali pake hapalikumbuki tena.
17 Lakini kutoka milele hata milele
upendo wa Mwenyezi Mungu uko kwa wale wamchao,
nayo haki yake kwa watoto wa watoto wao:
18 kwa wale walishikao agano lake
na kukumbuka kuyatii mausia yake.
19 Mwenyezi Mungu ameweka imara kiti chake cha enzi mbinguni,
na ufalme wake unatawala vitu vyote.
20 Mhimidini Mwenyezi Mungu, enyi malaika wake,
ninyi mlio mashujaa, mnaozitii amri zake,
ninyi mnaotii neno lake.
21 Mhimidini Mwenyezi Mungu, ninyi jeshi lake lote la mbinguni,
ninyi watumishi wake mnaofanya mapenzi yake.
22 Mhimidini Mwenyezi Mungu, enyi kazi zake zote
kila mahali katika milki yake.
Ee nafsi yangu, umhimidi Mwenyezi Mungu.