Zaburi 141
Maombi ya kuhifadhiwa dhidi ya uovu
Zaburi ya Daudi.
Ee Mwenyezi Mungu, ninakuita, njoo kwangu hima.
Sikia sauti yangu ninapokuita.
Maombi yangu na yafike mbele zako kama uvumba;
kuinua mikono yangu juu na kuwe kama dhabihu ya jioni.
 
Ee Mwenyezi Mungu, weka mlinzi kinywani mwangu,
weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu.
Usiuache moyo wangu uvutwe katika jambo baya,
nisije nikashiriki katika matendo maovu
pamoja na watu watendao mabaya,
wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa.
 
Mtu mwenye haki na anipige: ni jambo la huruma;
na anikemee: ni mafuta kichwani mwangu.
Kichwa changu hakitalikataa.
 
Hata hivyo, maombi yangu daima
ni kinyume cha watenda maovu.
Watawala wao watatupwa chini
kutoka majabali,
waovu watajifunza kwamba maneno yangu
yalikuwa kweli.
Watasema, “Kama mtu anavyolima na kuvunja ardhi,
ndivyo mifupa yetu imetawanywa kwenye mlango wa kaburi.”
 
Lakini nimekaza macho yangu kwako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi,
ndani yako nimekimbilia, usiniache nife.
Niepushe na mitego waliyonitegea,
kutokana na mitego iliyotegwa na watenda maovu.
10 Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe,
wakati mimi ninapita salama.