Zaburi 143
Maombi ya kuokolewa dhidi ya adui
Zaburi ya Daudi.
1 Ee Mwenyezi Mungu, sikia sala yangu,
sikiliza kilio changu unihurumie;
katika uaminifu na haki yako
njoo unisaidie.
2 Usimhukumu mtumishi wako,
kwa kuwa hakuna mtu aliye hai
mwenye haki mbele zako.
3 Adui hunifuatilia,
hunipondaponda chini;
hunifanya niishi gizani
kama wale waliokufa zamani.
4 Kwa hiyo roho yangu inazimia ndani yangu,
moyo wangu ndani yangu unakata tamaa.
5 Nakumbuka siku za zamani;
natafakari juu ya kazi zako zote,
naangalia juu ya kazi
ambazo mikono yako imezifanya.
6 Nanyoosha mikono yangu kwako,
nafsi yangu inakuonea kiu kama ardhi kame.
7 Ee Mwenyezi Mungu, unijibu haraka,
roho yangu inazimia.
Usinifiche uso wako,
ama sivyo nitafanana na wale wanaoshuka shimoni.
8 Asubuhi uniletee neno la upendo wako usiokoma,
kwa kuwa nimeweka tumaini langu kwako.
Nioneshe njia nitakayoiendea,
kwa kuwa kwako nainua nafsi yangu.
9 Ee Mwenyezi Mungu, uniokoe na adui zangu,
kwa kuwa nimejificha kwako.
10 Nifundishe kufanya mapenzi yako,
kwa maana wewe ndiwe Mungu wangu,
Roho wako mwema na aniongoze
katika nchi tambarare.
11 Ee Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya jina lako, hifadhi maisha yangu,
kwa haki yako nitoe katika taabu.
12 Kwa upendo wako usiokoma,
nyamazisha adui zangu;
waangamize watesi wangu wote,
kwa kuwa mimi ni mtumishi wako.