Zaburi 146
Kumsifu Mwenyezi Mungu mwokozi
1 Msifuni Mwenyezi Mungu!*kwa Kiebrania ni Hallelu Yah; pia 146:10.
Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi Mungu,
2 Nitamsifu Mwenyezi Mungu maisha yangu yote;
nitamwimbia Mungu wangu sifa
wakati wote ningali hai.
3 Usiweke tumaini lako kwa wakuu,
kwa wanadamu ambao hufa,
ambao hawawezi kuokoa.
4 Roho yao itokapo hurudi mavumbini,
siku hiyo hiyo mipango yao yote hukoma.
5 Heri yeye ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake,
ambaye tumaini lake ni katika Mwenyezi Mungu, Mungu wake,
6 Muumba wa mbingu na nchi,
na bahari na vyote vilivyomo:
Mwenyezi Mungu anayedumu kuwa mwaminifu
milele na milele.
7 Naye huwapatia haki waliodhulumiwa,
na kuwapa wenye njaa chakula.
Mwenyezi Mungu huwaweka wafungwa huru,
8 Mwenyezi Mungu huwafumbua vipofu macho,
Mwenyezi Mungu huwainua waliolemewa na mizigo yao,
Mwenyezi Mungu huwapenda wenye haki.
9 Mwenyezi Mungu huwalinda wageni
na kuwategemeza yatima na wajane,
lakini hupinga njia za waovu.
10 Mwenyezi Mungu atamiliki milele,
Mungu wako, ee Sayuni,
kwa vizazi vyote.
Msifuni Mwenyezi Mungu.