Ufunuo
1
Utangulizi
Ufunuo wa Isa Al-Masihi aliopewa na Mungu ili awaoneshe watumishi wake mambo ambayo ni lazima yatukie hivi karibuni. Alijulisha mambo haya kwa kumtuma malaika wake kwa Yohana mtumishi wake, ambaye anashuhudia kuhusu kila kitu alichokiona, yaani neno la Mungu na ushuhuda wa Isa Al-Masihi. Amebarikiwa yeye asomaye maneno ya unabii huu, na wamebarikiwa wale wanaoyasikia na kuyatia moyoni yale yaliyoandikwa humo, kwa sababu wakati umekaribia.
 
Salamu kwa makundi saba ya waumini
Yohana.
Kwa makundi saba ya waumini yaliyo jimbo la Asia.
Neema na amani ziwe kwenu kutoka kwake aliyeko, aliyekuwako, na atakayekuja, na kutoka kwa wale roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi, na kutoka kwa Isa Al-Masihi, aliye shahidi mwaminifu, mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, mtawala wa wafalme wa dunia.
Kwake yeye anayetupenda na aliyetuweka huru kutoka dhambi zetu kwa damu yake, na akatufanya sisi kuwa ufalme na makuhani, ili tumtumikie Mungu wake ambaye ni Baba*Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yake. Utukufu na uwezo ni vyake milele na milele! Amen.
“Tazama! Anakuja na mawingu,”
na “kila jicho litamwona,
hata wale waliomchoma”;
na makabila yote duniani
“yataomboleza kwa sababu yake.”
Naam, ndivyo itakavyokuwa! Amen.
 
“Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mwenyezi Mungu, “aliyeko, aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.”
 
Maono ya Al-Masihi
Mimi, Yohana, ndugu yenu ninayeshiriki pamoja nanyi mateso katika Isa na katika ufalme na uvumilivu katika saburi, nilikuwa katika kisiwa cha Patmo kwa ajili ya neno la Mungu na ushuhuda wa Isa. 10 Katika Siku ya Bwana, nilikuwa katika Roho wa Mungu na nikasikia sauti kubwa kama ya baragumu nyuma yangu 11 ikisema, “Andika kwenye kitabu haya yote unayoyaona, kisha uyapeleke kwa makundi saba ya waumini: kwa Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”
12 Ndipo nikageuka ili nione ni sauti ya nani iliyokuwa ikisema nami. Nami nilipogeuka, nikaona vinara saba vya taa vya dhahabu, 13 na katikati ya vile vinara vya taa, alikuwamo mtu kama Mwana wa Adamu, akiwa amevaa joho refu, na mkanda wa dhahabu ukiwa umefungwa kifuani mwake. 14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu, nyeupe kama theluji, nayo macho yake yalikuwa kama mwali wa moto. 15 Nyayo zake zilikuwa kama shaba inayong’aa katika tanuru la moto, nayo sauti yake ilikuwa kama mngurumo wa maji mengi. 16 Katika mkono wake wa kuume alishika nyota saba, na kinywani mwake ulitoka upanga mkali wenye makali kuwili. Uso wake ulikuwa kama jua liking’aa kwa nguvu zake zote.
17 Nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama aliyekufa. Ndipo akauweka mkono wake wa kuume juu yangu na kusema: “Usiogope, Mimi ndiye wa Kwanza na wa Mwisho. 18 Mimi ni Yeye Aliye Hai, niliyekuwa nimekufa, na tazama, ni hai milele na milele! Nami ninazo funguo za mauti na KuzimuKuzimu kwa Kiyunani ni Hades, yaani mahali pa wafu..
19 “Basi andika mambo uliyoyaona, yaliyopo na yale yatakayotukia baada ya haya. 20 Kuhusu siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa yale makundi saba ya waumini, navyo vile vinara saba ni hayo makundi saba.

*1:6 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.

1:18 Kuzimu kwa Kiyunani ni Hades, yaani mahali pa wafu.