19
Shangwe huko mbinguni
1 Baada ya haya nikasikia sauti kama ya umati mkubwa mbinguni wakipaza sauti na kusema:
“Haleluya!
Wokovu na utukufu na uweza ni vya Mungu wetu,
2 kwa maana hukumu zake
ni za kweli na za haki.
Amemhukumu yule kahaba mkuu
aliyeuharibu ulimwengu kwa uzinzi wake.
Mungu amemlipiza kisasi
kwa ajili ya damu ya watumishi wake.”
3 Wakasema tena kwa sauti kuu:
“Haleluya!
Moshi wake huyo kahaba unapanda juu
milele na milele.”
4 Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wanne wenye uhai wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti kuu:
“Amen, Haleluya!”
5 Kisha sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi, ikisema:
“Msifuni Mungu wetu,
ninyi watumishi wake wote,
ninyi nyote mnaomcha,
wadogo kwa wakubwa!”
6 Kisha nikasikia sauti kama ya umati mkubwa, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi wakipaza sauti na kusema:
“Haleluya!
Kwa maana Bwana Mungu wetu Mwenyezi anatawala.
7 Tufurahi, tushangilie
na kumpa utukufu!
Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia
na bibi arusi wake amejiweka tayari.
8 Akapewa kitani safi,
inayong’aa na nzuri,
ili avae.”
(Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya watakatifu.)
9 Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndio maneno ya kweli ya Mungu.”
10 Ndipo nikaanguka kifudifudi miguuni pake ili kumwabudu, lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi pia ni mtumishi mwenzako pamoja na ndugu zako walio na ushuhuda wa Isa. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Isa ndio roho ya unabii.”
Aliyepanda farasi mweupe
11 Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye yeye aliyempanda aliitwa Mwaminifu na Kweli. Yeye huhukumu kwa haki na kufanya vita. 12 Macho yake ni kama miali ya moto na juu ya kichwa chake kuna taji nyingi. Ana jina lililoandikwa ambalo hakuna mtu yeyote anayelijua isipokuwa yeye mwenyewe. 13 Amevaa joho lililoloweshwa katika damu, na Jina lake ni Neno la Mungu. 14 Majeshi ya mbinguni walikuwa wakimfuata, wakiwa wamepanda farasi weupe, hali wamevaa mavazi ya kitani safi, nyeupe na nzuri. 15 Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao kwa huo atayaangusha mataifa. “Atayatawala kwa fimbo yake ya utawala ya chuma.” Hulikanyaga shinikizo la ghadhabu ya Mungu Mwenyezi. 16 Kwenye joho lake na paja lake pameandikwa jina hili:
Mfalme wa wafalme
na Bwana wa mabwana.
Mnyama na majeshi yake washindwa
17 Nami nikamwona malaika amesimama ndani kwenye jua, naye akaita ndege wote warukao angani kwa sauti kuu, “Njooni, kusanyikeni kwa ajili ya karamu kubwa ya Mungu, 18 ili mpate kula nyama ya wafalme na ya majemadari, ya mashujaa, ya farasi na ya wapanda farasi, nyama ya wanadamu, wote walio huru na watumwa, wadogo kwa wakubwa.”
19 Kisha nikamwona yule mnyama na wafalme wa dunia pamoja na majeshi yao wakiwa wamekusanyika pamoja ili kufanya vita dhidi ya yule aliyempanda farasi pamoja na jeshi lake. 20 Lakini yule mnyama akakamatwa pamoja na huyo nabii wa uongo aliyekuwa amefanya ishara kwa niaba ya huyo mnyama, ambaye kwa ishara hizi aliwadanganya wale waliopokea chapa ya huyo mnyama na kuiabudu sanamu yake. Hawa wawili wakatupwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti. 21 Wale waliosalia waliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule aliyekuwa amempanda farasi nao ndege wote wakajishibisha kwa nyama yao.