3
Uaminifu wa Mwenyezi Mungu
1 Basi kuna faida gani kuwa Myahudi? Au kuna thamani gani katika tohara? 2 Kuna faida kubwa kwa kila namna! Kwanza kabisa, Wayahudi wamekabidhiwa maneno halisi ya Mungu.
3 Ingekuwaje kama wengine hawakuwa na imani? Je, kutokuamini kwao kungebatilisha uaminifu wa Mungu? 4 La hasha! Mungu na aonekane mwenye haki, na kila mwanadamu kuwa mwongo, kama ilivyoandikwa:
“Ili uthibitike kuwa wa kweli unaponena,
na ukashinde unapotoa hukumu.”
5 Lakini ikiwa uovu wetu unathibitisha haki ya Mungu waziwazi, tuseme nini basi? Je, Mungu kuileta ghadhabu yake juu yetu ni kwamba yeye si mwenye haki? (Nanena kibinadamu.) 6 La hasha! Kama hivyo ndivyo ilivyo, Mungu angewezaje kuhukumu ulimwengu? 7 Mtu aweza kuuliza, “Kama uongo wangu unasaidia kuonesha kweli ya Mungu na kuzidisha utukufu wake, kwa nini basi mimi nahukumiwa kuwa mwenye dhambi?” 8 Nasi kwa nini tusiseme, kama wengine wanavyotusingizia kuwa tunasema, “Tutende maovu ili mema yapate kuja”? Wao wanastahili hukumu yao.
Wote wametenda dhambi
9 Tusemeje basi? Je, sisi ni bora kuliko wao? La hasha! Kwa maana tumekwisha kuhakikisha kwa vyovyote kwamba Wayahudi na watu wa Mataifa wote wako chini ya nguvu ya dhambi. 10 Kama ilivyoandikwa:
“Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja.
11 Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu,
hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu.
12 Wote wamepotoka,
wote wameoza pamoja;
hakuna atendaye mema,
naam, hakuna hata mmoja.”
13 “Makoo yao ni makaburi wazi;
kwa ndimi zao wao hufanya udanganyifu.”
“Sumu ya nyoka iko midomoni mwao.”
14 “Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.”
15 “Miguu yao ina haraka kumwaga damu;
16 maangamizi na taabu viko katika njia zao,
17 wala njia ya amani hawaijui.”
18 “Hakuna hofu ya Mungu machoni pao.”
19 Basi tunajua kwamba chochote sheria inachosema, inawaambia wale walio chini ya sheria ili kila kinywa kinyamazishwe na ulimwengu wote uwajibike kwa Mungu. 20 Kwa hiyo hakuna binadamu hata mmoja atakayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo ya sheria, kwa maana sheria hutufanya tuitambue dhambi.
Haki kupitia kwa imani
21 Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Torati na Manabii wanaishuhudia. 22 Haki hii inayotoka kwa Mungu hupatikana kwa Isa Al-Masihi kwa wote wanaomwamini. Kwa maana hapo hakuna tofauti, 23 kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, 24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kupitia kwa ukombozi ulio katika Al-Masihi Isa. 25 Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kupitia kwa imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake, Mungu aliziachilia bila adhabu zile dhambi zilizotangulia kufanywa. 26 Alifanya hivyo ili kuonesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Isa.
Umuhimu wa kuwa na imani
27 Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La, bali kwa ile sheria ya imani. 28 Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kupitia kwa imani wala si kwa matendo ya sheria. 29 Je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi peke yao? Je, yeye si Mungu wa watu wa Mataifa pia? Naam, yeye ni Mungu wa watu wa Mataifa pia. 30 Basi kwa kuwa kuna Mungu mmoja tu, atawahesabia haki wale waliotahiriwa kwa imani na wale wasiotahiriwa kwa imani hiyo hiyo. 31 Je, basi ni kwamba tunaibatilisha sheria kwa imani hii? La, hasha! Badala yake tunaithibitisha sheria.