7
Kufunguliwa kutoka kwa Torati
1 Ndugu zangu, sasa ninasema na wale wanaoijua Torati: Je, hamjui kwamba Torati ina mamlaka juu ya mtu wakati akiwa hai tu? 2 Kwa mfano, mwanamke aliyeolewa amefungwa kwa mumewe wakati akiwa hai, lakini yule mume akifa, yule mwanamke amefunguliwa kutoka sheria ya ndoa. 3 Hivyo basi, kama huyo mwanamke ataolewa na mwanaume mwingine wakati mumewe akiwa bado yuko hai, ataitwa mzinzi. Lakini kama mumewe akifa, mwanamke huyo hafungwi tena na sheria ya ndoa, naye akiolewa na mtu mwingine haitwi mzinzi.
4 Vivyo hivyo, ndugu zangu, ninyi mmeifia Torati kupitia kwa mwili wa Al-Masihi, ili mweze kuwa mali ya mwingine, yeye ambaye alifufuliwa kutoka kwa wafu, ili tupate kuzaa matunda kwa Mungu. 5 Kwa maana tulipokuwa tunatawaliwa na asili ya dhambi, tamaa za dhambi zilizochochewa na Torati zilikuwa zikitenda kazi katika miili yetu, hivyo tulizaa matunda ya mauti. 6 Lakini sasa, kwa kufia kile kilichokuwa kimetufunga kwanza, tumewekwa huru kutokana na Torati ili tutumike katika njia mpya ya Roho wa Mungu, wala si katika njia ya zamani ya Torati iliyoandikwa.
Torati na dhambi
7 Tuseme nini basi? Kwamba Torati ni dhambi? La, hasha! Lakini singejua dhambi isipokuwa kwa sababu ya Torati. Singejua kutamani ni nini kama Torati haikusema, “Usitamani.” 8 Lakini dhambi ilipata nafasi katika amri, nayo ikazaa kila aina ya tamaa ndani yangu. Kwa maana pasipo sheria, dhambi imekufa. 9 Mwanzoni nilikuwa hai pasipo sheria; lakini amri ilipokuja, dhambi ikawa hai, nami nikafa. 10 Nikaona kwamba ile amri iliyokusudiwa kuleta uzima, ilileta mauti. 11 Kwa maana dhambi kwa kupata nafasi katika amri, ilinidanganya, na kupitia katika hiyo amri, ikaniua. 12 Hivyo basi, Torati yenyewe ni takatifu, na amri ni takatifu na ya haki, tena ni njema.
13 Je, kile kilicho chema basi kilikuwa mauti kwangu? La, hasha! Lakini ili dhambi itambuliwe kuwa ni dhambi, ilileta mauti ndani yangu kupitia kile kilichokuwa chema, ili kupitia kwa amri dhambi izidi kuwa mbaya kupita kiasi.
Mgongano wa ndani
14 Kwa maana tunajua kwamba Torati ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kimwili nikiwa nimeuzwa kwenye utumwa wa dhambi. 15 Sielewi nitendalo, kwa maana lile ninalotaka kulitenda, silitendi, lakini ninatenda lile ninalolichukia. 16 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, ni kwamba ninakubali kuwa Torati ni njema. 17 Lakini, kwa kweli si mimi tena nitendaye lile nisilotaka bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu. 18 Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote linalokaa ndani yangu, yaani katika asili yangu ya dhambi. Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda. 19 Sitendi lile jema nitakalo kutenda, bali lile baya nisilolitaka, ndilo nitendalo. 20 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu.
21 Hivyo naiona Torati ikitenda kazi. Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo. 22 Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia Torati ya Mungu. 23 Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu. 24 Ole wangu, mimi maskini! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?
25 Namshukuru Mungu anayeniokoa kupitia kwa Isa Al-Masihi Bwana wetu!
Hivyo basi, mimi mwenyewe kwa akili zangu ni mtumwa wa Torati ya Mungu, lakini katika asili ya dhambi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.