15
Usijipendeze mwenyewe tu
Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe. Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani. Kwa maana hata Al-Masihi hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.” Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini.
Mungu atoaye saburi na faraja awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Al-Masihi Isa, ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba*Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. wa Bwana wetu Isa Al-Masihi.
Injili sawa kwa Wayahudi na kwa watu wa Mataifa
Karibishaneni ninyi kwa ninyi kama Al-Masihi alivyowakaribisha ninyi ili kumletea Mungu utukufu. Kwa maana nawaambia kwamba Al-Masihi amekuwa mtumishi kwa wale waliotahiriwa ili kuonesha kweli ya Mungu, na kuthibitisha zile ahadi walizopewa baba zetu wa zamani, na pia ili watu wa Mataifa wamtukuze Mungu kwa rehema zake. Kama ilivyoandikwa:
“Kwa hiyo nitakutukuza kati ya watu wa Mataifa;
nitaliimbia sifa jina lako.”
10 Tena yasema,
“Enyi watu wa Mataifa, furahini
pamoja na watu wa Mungu.”
11 Tena,
“Msifuni Mwenyezi Mungu, ninyi watu wa Mataifa wote,
na kumwimbia sifa, enyi watu wote.”
12 Tena Isaya anasema,
“Shina la Yese litachipuka,
yeye atakayeinuka ili kuyatawala mataifa.
Watu wa Mataifa watamtumaini.”
13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu wa Mungu.
Paulo mhudumu wa watu wa Mataifa
14 Ndugu zangu, mimi mwenyewe ninasadiki kwamba mmejaa wema, mkijazwa ufahamu wote na mnaweza kufundishana ninyi kwa ninyi. 15 Hata hivyo, nimewaandikia kwa ujasiri vipengele kadha wa kadha katika waraka huu ili kuwakumbusha tena kuvihusu, kutokana na ile neema Mungu aliyonipa 16 niwe mhudumu wa Al-Masihi Isa kwa watu wa Mataifa. Alinipa huduma ya kikuhani ya kutangaza Injili ya Mungu, ili watu wa Mataifa wapate kuwa dhabihu inayokubalika na Mungu, kwa kutakaswa na Roho wa Mungu.
17 Kwa hiyo ninajisifu katika Al-Masihi Isa, kwenye utumishi wangu kwa Mungu. 18 Kwa maana sitathubutu kusema kitu chochote zaidi ya kile ambacho Al-Masihi amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu wa Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya, 19 kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake hadi Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Al-Masihi kwa ukamilifu. 20 Hivyo imekuwa nia yangu kuhubiri Injili pale ambapo Al-Masihi hajajulikana, ili nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. 21 Lakini kama ilivyoandikwa:
“Wale ambao hawajahubiriwa habari zake wataona,
nao wale ambao hawajazisikia watafahamu.”
22 Hii ndiyo sababu nimezuiliwa mara nyingi nisiweze kuja kwenu.
Paulo apanga kwenda Rumi
23 Lakini sasa kwa kuwa hakuna nafasi zaidi kwa ajili yangu katika sehemu hii, ninatamani kuja kwenu kama ambavyo nimekuwa na shauku kwa miaka mingi. 24 Nimekusudia kufanya hivyo nitakapokuwa njiani kwenda Hispania. Natarajia kuwaona katika safari yangu na kusafirishwa nanyi hadi huko, baada ya kufurahia ushirika wenu kwa kitambo kidogo. 25 Ila sasa niko njiani kuelekea Yerusalemu kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu huko. 26 Kwa kuwa imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya maskini walio miongoni mwa watakatifu huko Yerusalemu. 27 Imewapendeza kufanya hivyo, naam, kwani ni wadeni wao. Kwa maana ikiwa watu wa Mataifa wameshiriki baraka za rohoni za Wayahudi, wao ni wadeni wa Wayahudi, ili Wayahudi nao washiriki baraka zao za mambo ya mwilini. 28 Kwa hiyo baada ya kukamilisha kazi hii na kuhakikisha kuwa wamepokea kila kitu kilichokusanywa, nitapitia kwenu nikiwa njiani kwenda Hispania. 29 Ninajua kwamba nitakapokuja kwenu, nitakuja na wingi wa baraka za Al-Masihi.
30 Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Jina la Bwana wetu Isa Al-Masihi na kwa upendo wa Roho wa Mungu, kujiunga nami katika taabu zangu mkiniombea kwa Mungu. 31 Ombeni ili nipate kuokolewa mikononi mwa wale wasioamini walio Yudea, na kwamba utumishi wangu upate kukubaliwa na watakatifu wa huko Yerusalemu, 32 ili kwa mapenzi ya Mungu niweze kuja kwenu kwa furaha, nami niburudishwe pamoja nanyi. 33 Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amen.
 

*15:6 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu.