2
Maono ya tatu: Mtu mwenye kamba ya kupimia
1 Kisha nikatazama juu: pale mbele yangu palikuwa na mtu mwenye kamba ya kupimia mkononi mwake! 2 Nikamuuliza, “Unaenda wapi?”
Akanijibu, “Kupima Yerusalemu, kupata urefu na upana wake.”
3 Kisha malaika aliyekuwa akizungumza nami akaondoka, malaika mwingine akaja kukutana naye 4 na kumwambia: “Kimbia, umwambie yule kijana, ‘Yerusalemu utakuwa mji usio na kuta kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo. 5 Mimi mwenyewe nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘nami nitakuwa utukufu wake ndani yake.’
6 “Njooni! Njooni! Kimbieni mtoke katika nchi ya kaskazini,” asema Mwenyezi Mungu, “kwa kuwa nimewatawanya kwenye pande nne za mbingu,” asema Mwenyezi Mungu.
7 “Njoo, ee Sayuni! Kimbia, wewe ukaaye ndani ya Binti Babeli!” 8 Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: “Baada ya yeye kuniheshimu na kunituma mimi dhidi ya mataifa yaliyokuteka nyara, kwa kuwa yeyote awagusaye ninyi, anaigusa mboni ya jicho lake, 9 hakika nitauinua mkono wangu dhidi yao ili watumwa wao wawateke nyara. Ndipo mtajua kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amenituma.
10 “Shangilia na ufurahie, ee Binti Sayuni, kwa maana ninakuja, nami nitaishi miongoni mwenu,” asema Mwenyezi Mungu. 11 “Mataifa mengi yataunganishwa na Mwenyezi Mungu siku hiyo, nao watakuwa watu wangu. Nitaishi miongoni mwenu, nanyi mtajua kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amenituma kwenu. 12 Mwenyezi Mungu atairithi Yuda kama fungu lake katika nchi takatifu na atachagua tena Yerusalemu. 13 Tulieni mbele za Mwenyezi Mungu, enyi watu wote, kwa sababu ameinuka kutoka makao yake matakatifu.”