4
Maono ya tano: Kinara cha taa cha dhahabu na mizeituni miwili
1 Kisha malaika aliyezungumza nami akarudi na kuniamsha, kama mtu aamshwavyo kutoka usingizini. 2 Akaniuliza, “Unaona nini?”
Nikajibu, “Ninaona kinara cha taa cha dhahabu tupu, nacho kina bakuli juu yake na taa saba juu yake, tena iko mirija saba ya kuleta mafuta, kwenye taa zote zilizo juu yake. 3 Pia kuna mizeituni miwili karibu yake, mmoja upande wa kuume wa bakuli na mwingine upande wa kushoto.”
4 Nikamuuliza malaika aliyezungumza nami, “Hivi ni vitu gani, bwana wangu?”
5 Akanijibu, “Hujui kuwa hivi ni vitu gani?”
Nikajibu, “Hapana, bwana wangu.”
6 Kisha akaniambia, “Hili ni neno la Mwenyezi Mungu kwa Zerubabeli: ‘Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa Roho wangu Mtakatifu,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
7 “Wewe ni kitu gani, ee mlima mkubwa sana? Mbele ya Zerubabeli wewe utakuwa ardhi tambarare. Kisha ataweka jiwe la juu kabisa, na watu wakishangilia na kusema, ‘Mungu libariki! Mungu libariki!’ ”
8 Kisha neno la Mwenyezi Mungu likanijia: 9 “Mikono ya Zerubabeli iliweka msingi wa Hekalu hili, mikono yake pia italimalizia. Kisha mtajua ya kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amenituma mimi kwenu.
10 “Ni nani atakayeidharau siku ya mambo madogo? Macho saba ya Mwenyezi Mungu, yanayozunguka dunia yote, yatashangilia yatakapoona jiwe la juu kabisa likiwa mkononi mwa Zerubabeli!”
11 Kisha nikamuuliza yule malaika, “Hii mizeituni miwili iliyo upande wa kuume na wa kushoto wa kinara cha taa ni nini?”
12 Tena nikamuuliza, “Haya matawi mawili ya mizeituni karibu na hiyo mirija miwili ya dhahabu inayomimina mafuta ya dhahabu ni nini?”
13 Akajibu, “Hujui kuwa haya ni nini?”
Nikamjibu, “Hapana, bwana wangu.”
14 Kwa hiyo akasema, “Hawa ni wawili ambao wamepakwa mafuta ili kumtumikia Bwana wa dunia yote.”