2
Hukumu dhidi ya mataifa 
 Dhidi ya Yuda 
  1 Kusanyikeni pamoja, kusanyikeni pamoja,  
enyi taifa lisilo na aibu,   
 2 kabla wakati ulioamriwa haujafika  
na siku ile inayopeperusha kama makapi,  
kabla hasira kali ya Mwenyezi Mungu haijaja juu yenu,  
kabla siku ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu  
haijaja juu yenu.   
 3 Mtafuteni Mwenyezi Mungu, enyi nyote wanyenyekevu wa nchi,  
ninyi ambao hufanya lile analoamuru.  
Tafuteni haki, tafuteni unyenyekevu;  
labda mtahifadhiwa  
siku ya hasira ya Mwenyezi Mungu.   
Dhidi ya Ufilisti 
  4 Gaza utaachwa  
na Ashkeloni utaachwa magofu.  
Wakati wa adhuhuri Ashdodi utaachwa mtupu,  
na Ekroni utang’olewa.   
 5 Ole wenu ninyi ambao mnaishi kando ya bahari,  
enyi Wakerethi;  
neno la Mwenyezi Mungu liko dhidi yenu,  
ee Kanaani, nchi ya Wafilisti.  
“Mimi nitawaangamiza,  
na hakuna atakayebaki.”   
 6 Nchi iliyo karibu na bahari itakuwa malisho  
yenye visima vya wachungaji,  
na mazizi ya kondoo.   
 7 Itakuwa mali ya mabaki ya nyumba ya Yuda,  
hapo watapata malisho.  
Wakati wa jioni watajilaza chini  
katika nyumba za Ashkeloni.  
Mwenyezi Mungu, Mungu wao, atawatunza,  
naye atawarudishia wafungwa wao.   
Dhidi ya Moabu na Amoni 
  8 “Nimeyasikia matukano ya Moabu  
nazo dhihaka za Waamoni,  
ambao waliwatukana watu wangu  
na kutoa vitisho dhidi ya nchi yao.   
 9 Hakika, kama niishivyo,”  
asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,  
Mungu wa Israeli,  
“hakika Moabu itakuwa kama Sodoma,  
Waamoni kama Gomora:  
mahali pa magugu na mashimo ya chumvi,  
nchi ya ukiwa milele.  
Mabaki ya watu wangu watawateka nyara;  
mabaki ya taifa langu watarithi nchi yao.”   
 10 Hiki ndicho watarudishiwa kwa ajili ya kiburi chao,  
kwa kutukana na kudhihaki  
watu wa Mwenyezi Mungu,  
Mungu wa majeshi ya mbinguni.   
 11 Mwenyezi Mungu atakuwa wa kuhofisha kwao  
atakapoangamiza miungu yote ya nchi.  
Mataifa katika kila pwani yatamwabudu,  
kila moja katika nchi yake.   
Dhidi ya Kushi 
  12 “Ninyi pia, ee Wakushi,  
mtauawa kwa upanga wangu.”   
Dhidi ya Ashuru 
  13 Mungu atanyoosha mkono wake dhidi ya kaskazini  
na kuangamiza Waashuru,  
akiiacha Ninawi ukiwa  
na pakame kama jangwa.   
 14 Makundi ya kondoo na ng’ombe yatajilaza pale,  
viumbe vya kila aina.  
Bundi wa jangwani na bundi waliao kwa sauti nyembamba  
wataishi juu ya nguzo zake.  
Mwangwi wa kuita kwao utapita madirishani,  
kifusi kitakuwa milangoni,  
boriti za mwerezi zitaachwa wazi.   
 15 Huu ndio mji uliotukuka na kuishi kwa furaha  
wakijisikia salama.  
Ulisema moyoni mwako,  
“Mimi ndimi, na wala hapana mwingine ila mimi.”  
Jinsi gani umekuwa gofu,  
mahali pa kulala wanyama pori!  
Wote wanaopita kando yake wanauzomea  
na kutikisa mkono kwa dharau.