Wakolosai
1
Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu, kwa waumini na ndugu waaminifu katika Kristo walioko Kolosai. Neema iwe kwenu, na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu. Tunatoa shukrani kwa Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, na tunawaombea mara kwa mara. Tumesikia imani yenu katika Yesu Kristo na upendo mlionao kwa wale wote waliotengwa kwa ajili ya Mungu. Mna upendo huu kwa sababu ya taraja la uhakika lililohifadhiwa mbinguni kwa ajili yenu. Mlisikia kuhusu taraja hiyo ya uhakika kabla katika neno la kweli, injili, ambayo imekuja kwenu. Injili hii inazaa tunda na inaenea ulimwenguni kote. Imekuwa ikifanya hivi ndani yenu pia tangu siku mlipoisikia na kujifunza kuhusu neema ya Mungu katika kweli. Hii ndiyo injili mliyojifunza kutoka kwa Epafra, mpendwa wetu mtumishi mwenzetu, ambaye ni mtumishi mwaminifu wa Kristo kwa niaba yetu. Epafra ameufanya ujulikane kwetu upendo wenu katika Roho. Kwa sababu ya upendo huu, tangu siku tuliposikia hivi, hatujaacha kuwaombea. Tumekuwa tukiomba kwamba mtajazwa na maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa kiroho. 10 Tumekuwa tukiomba kwamba mtatembea kwa ustahimilivu wa Bwana katika njia zipendezazo. Tumekuwa tukiomba kwamba mtazaa tunda katika kila tendo jema na kwamba mtakua katika maarifa ya Mungu. 11 Tunaomba mweze kutiwa nguvu katika kila uwezo kulingana na nguvu za utukufu wake katika uvumilivu na ustahimilivu wote. 12 Tunaomba kwamba, kwa furaha, mtatoa shukrani kwa Baba, aliyewafanya ninyi mweze kuwa na sehemu katika urithi wa waumini katika nuru. 13 Ametuokoa kutoka katika utawala wa giza na kutuhamishia katika ufalme wa Mwana wake mpendwa. 14 Katika Mwanae tuna ukombozi, msamaha wa dhambi. 15 Mwana ni mfano wa Mungu asiyeonekana. Ni mzaliwa wa kwanza wa uumbaji wote. 16 Kwakuwa kwa yeye vitu vyote viliumbwa, vile vilivyoko mbinguni na vilivyoko duniani, vitu vinavyoonekana na visivyoonekana. ikiwa ni vya enzi au mamlaka au utawala au wenye nguvu, vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake. 17 Yeye amekuwepo kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja. 18 Na yeye ndiye kichwa cha mwili yaani kanisa, yeye ni mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka miongoni mwa wafu, hivyo, ana nafasi ya kwanza miongoni mwa vitu vyote. 19 Kwa kuwa Mungu alipendezwa kwamba utimilifu wake wote uishi ndani yake, 20 na kupatanisha vitu vyote kwake kwa njia ya Mwanawe. Mungu alifanya amani kupitia damu ya msalaba wake. Mungu alipatanisha vitu vyote kwake mwenyewe, ikiwa ni vitu vya duniani au vitu vya mbinguni. 21 Nanyi pia, kwa wakati mmoja mlikuwa wageni kwa Mungu na mlikuwa maadui wake katika akili na matendo maovu. 22 Lakini sasa amewapatanisha ninyi kwa mwili wake kupitia kifo. Alifanya hivi ili kuwaleta ninyi watakatifu, wasio na lawama na bila dosari mbele yake, 23 kama mkiendelea katika imani, mliyoimarishwa na kuwa thabiti, pasipo kuondoshwa mbali kutoka kwenye taraja la ujasiri la injili mliyoisikia. Hi ndiyo injili iliyotangazwa kwa kila mtu aliyeumbwa chini ya mbingu. Hii ndiyo injili ambayo kwayo mimi, Paulo, nimekuwa mtumishi. 24 Sasa nafurahia mateso yangu kwa ajili yenu. Nami natimiliza katika mwili wangu kinachopungua kwa mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni kanisa. 25 Mimi ni mtumishi wa kanisa hili, sawasawa na wajibu niliopewa kutoka kwa Mungu kwa ajili yenu, kulijaza neno la Mungu. 26 Huu ni ukweli wa siri iliyokuwa imefichwa kwa miaka mingi na kwa vizazi. Lakini sasa imefunuliwa kwa wote waaminio katika Yeye. 27 Ni kwa wale ambao Mungu alitaka kufunua kulivyo utajiri wa utukufu wa siri ya ukweli huu miongoni mwa Mataifa. Ni kwamba Kristo yumo ndani yenu, ujasiri wa utukufu ujao. 28 Huyu ndiye tunayemtangaza. Tunamwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu kwa hekima yote, ili kwamba tumlete kila mtu mkamilifu katika Kristo. 29 Kwa jili hii, mimi najibidisha na kujitahidi kulingana na nguvu yake ifanyayo kazi ndani yangu katika uweza.