34
1 Zaidi ya hayo, Elihu aliendelea kusema: 2 “Sikilizeni maneno yangu, ninyi watu wenye hekima; nisikieni, ninyi mlio na maarifa. 3 Kwa kuwa sikio huyajaribu maneno kama ambavyo kaakaa huonja chakula. 4 Na tujichagulie sisi wenyewe yale yenye adili: na tujigundulie miongoni mwetu yale yaliyo mazuri. 5 Kwa kuwa Ayubu amesema, 'mimi ni mwenye haki, lakini Mungu ameondoa haki zangu. 6 Pamoja na haki zangu, ninaangaliwa kama mwongo. Kidonda changu hakiponyeki, ingawa mimi sina dhambi.' 7 Ni mtu gani aliye kama Ayubu ambaye hunywa dharau kama maji, 8 ambaye huzunguka katika ushirika wa watu ambao ni waovu, na ambaye hutembea pamoja na watu waovu? 9 Kwa kuwa anasema, ' Hakuna faida kwa mtu kujifurahisha kwa kufanya mambo ambayo Mungu anayataka.' 10 Basi nisikilizeni mimi, enyi watu wenye ufahamu: na iwe mbali na Mungu kwamba atatenda uovu; 11 na iwe mbali na Mwenye enzi kwamba atatenda dhambi. Kwa kuwa humlipa mtu kutokana na kazi yake; na humfanya mtu apate thawabu za njia zake mwenyewe. 12 Kwa hakika, Mungu hatendi uovu, wala Mwenye nguvu hajaIpotosha haki. 13 Ni nani aliyemweka kuwa mtawala wa dunia? Ni nani aliyeiweka dunia yote chini yake? 14 Ikiwa aliweka makusudio yake juu yake mwenyewe, na kama amejikusanyia mwenyewe nafsi yake na pumzi yake, 15 basi miili yote itateketea pamoja; mwanadamu angerudi mavumbini tena. 16 Kama sasa mna ufahamu, sikilizeni haya; sikilizeni sauti ya maneno yangu. 17 Je yeye anayeichukia haki aweza kutawala? Je mtamhukumu Mungu kuwa ni mwenye makosa, ambaye ni mwenye haki na mwenye nguvu? 18 Mungu ambaye humwambia mfalme, ' Wewe ni mbaya; au huwaambia wenye kuheshimiwa, 'Ninyi ni waovu'? 19 Mungu ambaye haoneshi upendeleo kwa viongozi na ambaye hawakubali zaidi watu matajiri kuliko masikini, kwa kuwa wote ni kazi ya mikono yake. 20 Watakufa kwa muda mfupi; wakati wa usiku watu watatikiswa na watapita; watu wenye nguvu watatwaliwa mbali, lakini si kwa mikono ya wanadamu. 21 Kwa kuwa macho ya Mungu yako juu ya njia za mtu; anaziona hatua zake zote. 22 Hakuna giza, wala hakuna weusi mzito ambao watenda mabaya wanaweza kujificha wao wenyewe. 23 Kwa kuwa Mungu hahitaji kumchunguza mtu zaidi; wala hakuna haja kwa mtu yeyote kwenda mbele zake kwa hukumu. 24 Huwavunja vipande vipande watu wenye nguvu kwa ajili ya njia zao ambazo hazihitaji uchunguzi zaidi; huwaweka watu wengine katika nafasi zao. 25 Kwa namna hii ana maarifa juu ya matendo yao; huwatupa watu hawa wakati wa usiku; nao wameangamizwa. 26 Huwaua kwa matendo yao mabaya kama wakosaji dhahiri mbele za watu wengine 27 kwasababu wamegeuka na kuacha kumfuata yeye na wamekataa kuzisadiki njia zake zozote. 28 Na kwa namna hii, wamekifanya kilio cha watu masikini kimfikie; amekisikia kilio cha watu walioteswa. 29 Na wakati akaapo kimya, nani aweza kumhukumu kuwa mkosaji? Kama akiuficha uso wake, ni nani awezaye kumjua? Anatawala sawa sawa juu ya taifa na mtu pia, 30 ili kwamba watu wasiomjua Mungu wasije wakatawala, ili kwamba asiwepo mtu wa kuwanasa watu. 31 Fikiria mtu akimwambia Mungu, ' Mimi ni mwenye hatia kabisa, lakini sitatenda dhambi tena; 32 nifunze kile ambacho siwezi kukiona; nimetenda dhambi, lakini sitafanya tena.' 33 Je unadhani kwamba Mungu ataiadhibu dhambi ya mtu huyo, kwa kuwa unayachukia yale ambayo Mungu huyatenda? Ni lazima uchague, siyo mimi. Basi sema yale ambayo unayajua. 34 Watu wenye ufahamu wataniambia, kwa kweli, kila mtu mwenye hekima ambaye hunisikia atasema, 35 Ayubu anazungumza bila maarifa; maneno yake hayana hekima.' 36 Kama Ayubu alijaribiwa kwa kitu kidogo kabisa katika kesi yake kwasababu ya kuongea kwake kama watu waovu. 37 Kwa kuwa anaongeza uasi juu ya dhambi yake; anapiga makofi ya dharau kati yetu; anaweka maneno kinyume na Mungu.”