23
1 Kisha Yesu akauambia umati wa watu pamoja na wanafunzi wake,
2 “Walimu wa Sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kufafanua Sheria ya Mose.
3 Kwa hiyo shikeni na kutekeleza chochote watakachowaambieni. Lakini msiyaige matendo yao, maana hawatekelezi yale wanayoyahubiri.
4 Hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani, lakini wao wenyewe hawataki kunyosha hata kidole wapate kuibeba.
5 Wao hufanya matendo yao yote ili watu wawaone. Huvaa tepe zenye maandishi ya Sheria juu ya panda la uso na mikononi na hupanua pindo za makoti yao.
6 Hupenda nafasi za heshima katika karamu na viti vya heshima katika masunagogi.
7 Hupenda kusalimiwa kwa heshima sokoni na kupendelea kuitwa na watu: Mwalimu.
8 Lakini ninyi msiitwe kamwe Mwalimu, maana mwalimu wenu ni mmoja tu, nanyi nyote ni ndugu.
9 Wala msimwite mtu yeyote Baba hapa duniani, maana Baba yenu ni mmoja tu aliye mbinguni.
10 Wala msiitwe Viongozi, maana kiongozi wenu ni mmoja tu, ndiye Kristo.
11 Aliye mkubwa miongoni mwenu ni lazima awe mtumishi wenu.
12 Anayejikweza atashushwa, na anayejishusha atakwezwa.
13 “Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnaufunga mlango wa Ufalme wa mbinguni mbele ya macho ya watu. Ninyi wenyewe hamwingii ndani, wala hamwaruhusu wanaotaka kuingia waingie.
14 Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnawanyonya wajane na kujisingizia kuwa watu wema kwa kusali sala ndefu. Kwa sababu hiyo mtapata adhabu kali.
15 “Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumpata mtu mmoja afuate dini yenu. Mnapompata, mnamfanya astahili maradufu kwenda katika moto wa Jehanamu kuliko ninyi wenyewe.
16 “Ole wenu viongozi vipofu! Ninyi mwasema ati mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini akiapa kwa dhahabu ya Hekalu, kiapo hicho kinamshika.
17 Enyi vipofu wapumbavu! Kipi kilicho cha maana zaidi: dhahabu au Hekalu linalofanya hiyo dhahabu kuwa takatifu?
18 Tena mwasema ati mtu akiapa kwa madhabahu si kitu; lakini akiapa kwa zawadi iliyowekwa juu ya madhabahu, kiapo hicho humshika.
19 Enyi vipofu! Ni kipi kilicho cha maana zaidi: ile zawadi, au madhabahu ambayo hufanya hiyo zawadi kuwa takatifu?
20 Anayeapa kwa madhabahu ameapa kwa hiyo madhabahu, na kwa chochote kilichowekwa juu yake.
21 Na anayeapa kwa Hekalu ameapa kwa hilo Hekalu na pia kwa yule akaaye ndani yake.
22 Na anayeapa kwa mbingu ameapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa huyo aketiye juu yake.
23 Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnatoza watu zaka, hata juu ya majani yenye harufu nzuri, bizari na jira, na huku mnaacha mambo muhimu ya Sheria kama vile haki, huruma na imani. Haya ndiyo hasa mliyopaswa kuyazingatia bila kusahau yale mengine.
24 Viongozi vipofu! Mnatoa nzi katika kinywaji, lakini mnameza ngamia!
25 “Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafisha kikombe na bakuli kwa nje, lakini ndani mnaacha kumejaa vitu mlivyopata kwa unyang'anyi na uchoyo.
26 Mfarisayo kipofu! Kisafishe kikombe ndani kwanza na nje kutakuwa safi pia.
27 “Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mko kama makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa nje yanaonekana kuwa mazuri, lakini ndani yamejaa mifupa ya maiti na kila namna ya uchafu.
28 Hali kadhalika ninyi mnaonekana na watu kwa nje kuwa wema, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.
29 “Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya watu wema.
30 Mwasema: Kama sisi tungaliishi nyakati za wazee wetu hatungalishirikiana nao katika mauaji ya manabii!
31 Hivyo mnathibitisha ninyi wenyewe kwamba ninyi ni watoto wa watu waliowaua manabii.
32 Haya, kamilisheni ile kazi wazee wenu waliyoianza!
33 Enyi kizazi cha nyoka wenye sumu! Mnawezaje kuiepa hukumu ya moto wa Jehanamu?
34 Ndiyo maana mimi ninawapelekea ninyi manabii, watu wenye hekima na walimu; mtawaua na kuwasulubisha baadhi yao, na wengine mtawapiga viboko katika masunagogi yenu na kuwasaka katika kila mji.
35 Hivyo lawama yote itawapateni kwa ajili ya damu yote ya watu wema iliyomwagwa juu ya ardhi. Naam, tangu kuuawa kwa Abeli ambaye hakuwa na hatia, mpaka kuuawa kwa Zakariya, mwana wa Barakia, ambaye mlimuua Hekaluni kati ya patakatifu na madhabahu.
36 Nawaambieni kweli, kizazi hiki kitapata adhabu kwa sababu ya mambo haya.
37 “Yerusalemu, Ee Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako. Mara ngapi nimejaribu kuwakusanya watoto wako kwangu, kama vile kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka.
38 Haya basi, nyumba yako itaachwa mahame.
39 Nakwambia kweli, hutaniona tena mpaka wakati utakaposema: Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana.”