29
Kuweka Wakfu Makuhani
(Walawi 8:1-36)
“Hili ndilo utakalofanya ili kuwaweka wakfu makuhani ili wanitumikie mimi katika kazi ya ukuhani: Chukua fahali mchanga mmoja na kondoo dume wawili wasio na dosari. Kutokana na unga laini wa ngano usiotiwa chachu, tengeneza mikate na maandazi yaliyokandwa kwa mafuta, pamoja na mikate midogo myembamba. Viwekwe vyote ndani ya kikapu na kuvitoa pamoja na yule fahali na wale kondoo dume wawili. Kisha mlete Aroni na wanawe kwenye lango la Hema la Kukutania na uwaoshe kwa maji. Chukua yale mavazi na umvike Aroni koti, joho la kisibau na kisibau chenyewe pamoja na kile kifuko cha kifuani. Mfungie hicho kisibau kwa ule mshipi wa kiunoni uliosukwa kwa ustadi. Weka kilemba kichwani mwake na kuweka taji takatifu ishikamane na hicho kilemba. Chukua yale mafuta ya upako umimine juu ya kichwa chake. Walete wanawe na uwavike makoti, pia uwavike zile tepe za kichwani. Ndipo uwafunge Aroni na wanawe mishipi. Ukuhani ni wao kwa agizo la kudumu. Kwa njia hii utamweka wakfu Aroni na wanawe.
10 “Mlete yule fahali mbele ya Hema la Kukutania, naye Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake. 11 Mchinje huyo fahali mbele za Bwana kwenye mlango wa Hema la Kukutania. 12 Chukua sehemu ya damu ya huyo fahali na kuipaka kwenye pembe za hayo madhabahu kwa kidole chako, na damu iliyobaki uimwage sehemu ya chini ya madhabahu. 13 Kisha chukua mafuta yote ya huyo mnyama ya sehemu za ndani, yale yanayofunika ini, figo zote mbili pamoja na mafuta yake, uviteketeze juu ya madhabahu. 14 Lakini nyama ya huyo fahali na ngozi yake na matumbo yake utavichoma nje ya kambi. Hii ni sadaka ya dhambi.
15 “Chukua mmoja wa wale kondoo dume, naye Aroni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake. 16 Mchinje huyo kondoo dume, chukua damu yake na uinyunyize pande zote za hayo madhabahu. 17 Mkate huyo kondoo dume vipande vipande na usafishe sehemu za ndani pamoja na miguu, ukiviweka pamoja na kichwa na vipande vingine. 18 Kisha mteketeze huyo kondoo dume mzima juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana, harufu ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto.
19 “Mchukue yule kondoo dume mwingine, naye Aroni na wanawe waweke mikono yao juu ya kichwa chake. 20 Mchinje, uchukue sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye masikio ya Aroni na wanawe, kwenye vidole gumba vya mikono yao ya kuume, pia kwenye vidole gumba vya miguu yao ya kuume. Kisha nyunyiza hiyo damu pande zote za madhabahu. 21 Pia chukua sehemu ya damu iliyo juu ya madhabahu na sehemu ya mafuta ya upako, umnyunyizie Aroni na mavazi yake, pia wanawe na mavazi yao. Ndipo Aroni na wanawe pamoja na mavazi yao watakuwa wamewekwa wakfu.
22 “Chukua mafuta ya huyu kondoo dume, mafuta ya mkia, mafuta ya sehemu za ndani yale yanayofunika ini, figo zote mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kulia. (Huyo ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu.) 23 Kutoka kwenye kile kikapu chenye mikate iliyotengenezwa bila chachu, kilichoko mbele za Bwana, chukua mkate, andazi lililokandwa kwa mafuta na mkate mdogo mwembamba. 24 Viweke vitu hivi vyote mikononi mwa Aroni na wanawe na uviinue mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa. 25 Kisha vichukue vitu hivyo kutoka mikononi mwao, uviteketeze juu ya madhabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kupendeza kwa Bwana, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto. 26 Baada ya kuchukua kidari cha huyo kondoo dume wa kuwekwa wakfu kwa Aroni, kiinue mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa, nayo itakuwa fungu lako.
27 “Weka wakfu zile sehemu za kondoo dume aliyetumika kwa kumweka wakfu Aroni na wanawe: kidari kile kilichoinuliwa na lile paja lililotolewa. 28 Siku zote hili litakuwa fungu la kawaida kutoka kwa Waisraeli kwa ajili ya Aroni na wanawe. Hili ni toleo la Waisraeli watakalotoa kwa Bwana kutoka sadaka zao za amani.
29 “Mavazi matakatifu ya Aroni yatakuwa ya wazao wake ili kwamba waweze kutiwa mafuta na kuwekwa wakfu wakiwa wameyavaa. 30 Mwana atakayeingia mahali pake kuwa kuhani na kuja kwenye Hema la Kukutania kuhudumu katika Mahali Patakatifu atayavaa kwa siku saba.
31 “Chukua nyama ya huyo kondoo dume wa kuwaweka wakfu uipike katika Mahali Patakatifu. 32 Aroni na wanawe wataila ile nyama ya huyo kondoo dume pamoja na ile mikate iliyo kwenye hicho kikapu wakiwa hapo ingilio la Hema la Kukutania. 33 Watakula sadaka hizi ambazo upatanisho ulifanywa kwazo kwa ajili ya kuwaweka wakfu na kuwatakasa. Lakini hakuna mtu mwingine yeyote anayeruhusiwa kuvila, kwa sababu ni vitakatifu. 34 Ikiwa nyama yoyote ya huyo kondoo dume iliyotumika kwa kuwaweka wakfu au mkate wowote umebaki mpaka asubuhi, vichomwe. Kamwe visiliwe, kwa sababu ni vitakatifu.
35 “Hivyo utamfanyia Aroni na wanawe kila kitu kama vile nilivyokuamuru: Utachukua muda wa siku saba kuwaweka wakfu. 36 Utatoa dhabihu ya fahali kila siku kuwa sadaka ya dhambi ili kufanya upatanisho. Takasa madhabahu kwa kufanya upatanisho kwa ajili yake, nayo uitie mafuta na kuiweka wakfu. 37 Kwa muda wa siku saba fanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu na kuiweka wakfu. Ndipo madhabahu itakuwa takatifu sana na chochote kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.
38 “Kwa kawaida hiki ndicho utakachotoa juu ya madhabahu kila siku: wana-kondoo wawili wenye umri wa mwaka mmoja. 39 Utamtoa mmoja asubuhi na huyo mwingine jioni. 40 Pamoja na mwana-kondoo wa kwanza utatoa efa moja* ya unga wa ngano laini uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta yaliyokamuliwa, pamoja na robo ya hini ya divai kuwa sadaka ya kinywaji. 41 Huyo mwana-kondoo mwingine mtoe dhabihu wakati wa machweo pamoja na sadaka za unga na za kinywaji kama vile ulivyofanya asubuhi, kuwa harufu ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto.
42 “Kwa vizazi vijavyo itakuwa kawaida kutoa sadaka hii ya kuteketezwa kila mara kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za Bwana. Hapo ndipo nitakapokutana na ninyi na kusema nanyi, 43 Huko ndipo nitakapokutana na Waisraeli, nalo Hema la Kukutania litatakaswa na utukufu wangu.
44 “Kwa hiyo nitaliweka wakfu Hema la Kukutania pamoja na madhabahu, nami nitamweka wakfu Aroni na wanawe ili wanitumikie mimi katika kazi ya ukuhani. 45 Ndipo nitakapofanya makao miongoni mwa Waisraeli na kuwa Mungu wao. 46 Nao watajua kuwa Mimi Ndimi Bwana Mungu wao, aliyewatoa Misri ili nipate kufanya makao miongoni mwao. Mimi Ndimi Bwana Mungu wao.
* 29:40 Efa moja ni sawa na kilo 22. 29:40 Robo ya hini ni sawa na lita moja.