30
Madhabahu Ya Kufukizia Uvumba
(Kutoka 37:25-28)
“Tengeneza madhabahu kwa mbao za mshita kwa ajili ya kufukizia uvumba. Madhabahu hayo yawe mraba, urefu na upana wake dhiraa moja,* na kimo cha dhiraa mbili, nazo pembe zake zitakuwa kitu kimoja nayo. Funika hayo madhabahu juu na pande zote na pia pembe zake kwa dhahabu safi, na uifanyizie ukingo wa dhahabu kuizunguka. Tengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili ya madhabahu chini ya huo ukingo, ziwe mbili kila upande, za kushikilia hiyo mipiko itumikayo kuibebea madhabahu. Tengeneza mipiko kwa miti ya mshita na uifunike kwa dhahabu. Weka hayo madhabahu mbele ya lile pazia lililo mbele ya Sanduku la Ushuhuda, lililo mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya Sanduku la Ushuhuda, mahali ambapo nitakutana nawe.
“Itampasa Aroni kufukiza uvumba wenye harufu nzuri juu ya madhabahu kila siku asubuhi wakati anapowasha zile taa. Itampasa afukize uvumba tena wakati anapowasha taa wakati wa machweo ili uvumba ufukizwe daima mbele za Bwana kwa vizazi vijavyo. Usifukize uvumba mwingine wowote juu ya madhabahu haya au sadaka nyingine yoyote ya kuteketezwa wala sadaka ya nafaka, wala usimimine sadaka ya kinywaji juu yake. 10 Mara moja kwa mwaka Aroni atafanya upatanisho juu ya pembe za hayo madhabahu. Upatanisho huu wa mwaka lazima ufanywe kwa damu ya sadaka ya upatanisho kwa ajili ya dhambi kwa vizazi vijavyo. Ni takatifu sana kwa Bwana.”
Fedha Ya Upatanisho
11 Naye Bwana akamwambia Mose, 12 “Utakapowahesabu Waisraeli, kila mmoja lazima alipe kwa Bwana fidia kwa ajili ya nafsi yake wakati wa kuhesabiwa kwake. Ndipo hakutakuwa na pigo juu yao unapowahesabu. 13 Kila mmoja anayekwenda upande wa wale waliokwisha hesabiwa atatoa nusu shekeli, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, ambayo ina uzito wa gera ishirini.§ Hii nusu shekeli ni sadaka kwa Bwana. 14 Wote wale wanaovuka, wenye umri wa miaka ishirini au zaidi, watatoa sadaka kwa Bwana. 15 Matajiri hawatalipa zaidi ya nusu shekeli, nao maskini hawatatoa pungufu wakati mnatoa sadaka kwa Bwana kwa kufanya upatanisho wa nafsi zenu. 16 Utapokea fedha ya upatanisho kutoka kwa Waisraeli na uzitumie kwa ajili ya huduma ya Hema la Kukutania. Itakuwa ni ukumbusho kwa Waisraeli mbele za Bwana kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu.”
Sinia La Kunawia
17 Kisha Bwana akamwambia Mose, 18 “Tengeneza sinia la shaba lenye kitako cha shaba kwa ajili ya kunawia. Liweke kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, kisha uweke maji ndani yake. 19 Aroni na wanawe watanawa mikono na miguu yao kwa maji yatokayo katika hilo sinia. 20 Wakati wowote wanapoingia katika Hema la Kukutania, watanawa kwa maji ili kwamba wasije wakafa. Pia, wanapokaribia madhabahu ili kuhudumu kwa kuleta sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, 21 watanawa mikono na miguu yao ili kwamba wasije wakafa. Hii itakuwa ni amri ya kudumu kwa ajili ya Aroni na wazao wake kwa vizazi vijavyo.”
Mafuta Ya Upako
22 Kisha Bwana akamwambia Mose, 23 “Chukua vikolezi bora vifuatavyo: shekeli 500* za manemane ya maji, shekeli 250 za mdalasini wenye harufu nzuri, shekeli 250 za miwa yenye harufu nzuri, 24 shekeli 500 za aina nyingine ya mdalasini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, pia hini ya mafuta ya zeituni. 25 Vitengeneze vikolezi hivi kuwa mafuta matakatifu ya upako yenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Yatakuwa mafuta matakatifu ya upako. 26 Kisha yatumie kupaka hilo Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda, 27 meza na vifaa vyake vyote, kinara cha taa na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba, 28 madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote na sinia pamoja na kitako chake. 29 Utaviweka wakfu ili viwe vitakatifu sana na kila kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.
30 “Mtie Aroni na wanawe mafuta na uwaweke wakfu ili waweze kunitumikia katika kazi ya ukuhani. 31 Waambie Waisraeli, ‘Haya yatakuwa mafuta matakatifu yangu ya upako kwa vizazi vijavyo. 32 Usiyamimine juu ya miili ya wanadamu wala usitengeneze mafuta ya aina nyingine kwa utaratibu huu. Ni mafuta matakatifu na ni lazima myaone kuwa ni matakatifu. 33 Mtu yeyote atakayetengeneza manukato kama hayo na yeyote atakayeyamimina juu ya mtu yeyote ambaye si kuhani atakatiliwa mbali na watu wake.’ ”
Uvumba
34 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Chukua vikolezi vyenye harufu nzuri vifuatavyo: natafi, shekelethi, kelbena na uvumba safi vyote vikiwa na vipimo sawa, 35 pia tengeneza mchanganyiko wa uvumba wenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Utiwe chumvi ili upate kuwa safi na mtakatifu. 36 Saga baadhi yake kuwa unga na uweke mbele ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, mahali ambapo nitakutana nawe. Itakuwa takatifu sana kwenu. 37 Msitengeneze uvumba mwingine wowote wa namna hii kwa ajili yenu wenyewe; uoneni kuwa ni mtakatifu kwa Bwana. 38 Yeyote atakayetengeneza uvumba kama huu ili kufurahia harufu yake nzuri lazima akatiliwe mbali na watu wake.”
* 30:2 Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45. 30:2 Dhiraa mbili ni sawa na sentimita 90. 30:13 Nusu shekeli ni sawa na gramu 6. § 30:13 Gera 20 ni sawa na shekeli moja au gramu 12. * 30:23 Shekeli 500 ni sawa na kilo 6. 30:23 Shekeli 250 ni sawa na kilo 3. 30:24 Hini moja ni sawa na lita 4.