23
Hotuba Ya Nane Ya Ayubu
Ayubu Anajibu: Kulalamika Kwangu Ni Uchungu
Ndipo Ayubu akajibu:
“Hata leo malalamiko yangu ni chungu;
mkono wake ni mzito juu yangu hata nikiugua.
Laiti ningefahamu mahali pa kumwona;
laiti ningeweza kwenda mahali akaapo!
Ningeliweka shauri langu mbele zake,
na kukijaza kinywa changu na hoja.
Ningejua kwamba angenijibu nini,
na kuelewa lile ambalo angelisema.
Je, angenipinga kwa nguvu nyingi?
La, asingenigandamiza.
Hapo mtu mwadilifu angeweka shauri lake mbele zake,
nami ningeokolewa milele na mhukumu wangu.
 
“Lakini nikienda mashariki, hayupo;
nikienda magharibi, simpati.
Anapokuwa kazini pande za kaskazini, simwoni;
akigeukia kusini, nako simwoni hata kidogo.
10 Lakini anaijua njia niiendeayo;
akiisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.
11 Nyayo zangu zimefuata hatua zake kwa karibu;
nimeishika njia yake bila kukengeuka.
12 Sijaziacha amri zilizotoka midomoni mwake;
nimeyathamini maneno ya kinywa chake kuliko chakula changu cha kila siku.
 
13 “Lakini yeye husimama peke yake; ni nani awezaye kumpinga?
Yeye hufanya lolote atakalo.
14 Hutimiliza maagizo yake dhidi yangu,
na bado anayo mipango mingi kama hiyo ambayo ameiweka akiba.
15 Hiyo ndiyo sababu ninaingiwa na hofu mbele zake;
nifikiriapo haya yote ninamwogopa.
16 Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia;
yeye Mwenyezi amenitia hofu.
17 Hata hivyo sijanyamazishwa na giza,
wala kwa giza nene linalofunika uso wangu.