14
Watu wanaasi
Usiku ule watu wote wa jumuiya walipaza sauti zao na kulia kwa sauti kuu. Waisraeli wote wakanung’unika dhidi ya Musa na Haruni, na kusanyiko lote wakawaambia, “Laiti tungekuwa tumefia humo nchi ya Misri! Au humu kwenye hili jangwa! Kwa nini Mwenyezi Mungu anatuleta katika nchi hii ili tufe kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watachukuliwa kama nyara. Je, isingekuwa bora kwetu kurudi Misri?” Wakasemezana wao kwa wao, “Inatupasa kumchagua kiongozi na kurudi Misri.”
Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya kusanyiko lote la Waisraeli waliokusanyika hapo. Yoshua mwana wa Nuni na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwa watu wale walioenda kuipeleleza nchi, wakararua nguo zao, wakasema na kusanyiko lote la Waisraeli, wakawaambia, “Nchi tuliyopita kati yake kuipeleleza ni nzuri sana. Ikiwa Mwenyezi Mungu anapendezwa nasi, atatuongoza kuingia katika nchi ile, nchi inayotiririka maziwa na asali, naye atatupatia nchi hiyo. Ila tu msimwasi Mwenyezi Mungu. Wala msiwaogope watu wa nchi hiyo, kwa sababu tutawameza. Ulinzi wao umeondoka, lakini Mwenyezi Mungu yupo pamoja nasi. Msiwaogope.”
10 Lakini kusanyiko lote wakazungumza kuhusu kuwapiga kwa mawe. Ndipo utukufu wa Mwenyezi Mungu ukaonekana katika Hema la Kukutania kwa Waisraeli wote. 11 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Watu hawa watanidharau hadi lini? Wataendelea kukataa kuniamini mimi hadi lini, ingawa nimetenda ishara za miujiza miongoni mwao? 12 Nitawapiga kwa tauni na kuwaangamiza, lakini nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa lenye nguvu kuliko wao.”
13 Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Ndipo Wamisri watasikia juu ya jambo hili! Kwa uweza wako uliwapandisha watu hawa kutoka miongoni mwao. 14 Nao watawaambia wenyeji wa nchi hii jambo hili. Wao tayari wameshasikia kwamba wewe, Ee Mwenyezi Mungu, upo pamoja na watu hawa, na kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umeonekana uso kwa uso, nalo wingu lako hukaa juu yao. Tena wewe unawatangulia kwa nguzo ya wingu mchana na kwa nguzo ya moto usiku. 15 Ikiwa utawaua watu hawa wote mara moja, mataifa ambayo yamesikia taarifa hii kukuhusu wewe watasema, 16 ‘Mwenyezi Mungu alishindwa kuwaingiza watu hawa katika nchi aliyowaahidi kwa kiapo; hivyo akawaua jangwani.’
17 “Basi sasa nguvu za Bwana na zionekane, sawasawa na ulivyosema: 18 ‘Mwenyezi Mungu si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo na mwenye kusamehe dhambi na uasi. Lakini haachi kumwadhibu mwenye hatia, huadhibu watoto kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata kizazi cha tatu na cha nne.’ 19 Kwa kadiri ya upendo wako mkuu, usamehe dhambi ya watu hawa, kama vile ulivyowasamehe tangu walipotoka Misri hadi sasa.”
20 Mwenyezi Mungu akajibu, “Nimewasamehe kama ulivyoomba. 21 Hata hivyo, kwa hakika kama niishivyo, na kwa hakika kama utukufu wa Mwenyezi Mungu uijazavyo dunia yote, 22 hakuna hata mmoja wa watu hawa ambao waliuona utukufu wangu na ishara za miujiza niliyotenda huko Misri na huko jangwani, lakini ambaye hakunitii na akanijaribu mara hizi kumi, 23 hakuna hata mmoja wao atakayeona nchi niliyowaahidi baba zao kwa kiapo. Hakuna hata mmoja ambaye amenidharau atakayeiona. 24 Lakini kwa sababu mtumishi wangu Kalebu ana roho ya tofauti na ananifuata kwa moyo wote, nitamwingiza katika nchi aliyoiendea, nao wazao wake watairithi. 25 Kwa kuwa Waamaleki na Wakanaani wanaishi katika mabonde, kesho geukeni mwelekee jangwani kwa kufuata njia iendayo Bahari ya Shamu*.”
26 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni: 27 “Jumuiya hii ovu itanung’unika dhidi yangu hadi lini? Nimesikia malalamiko ya hawa Waisraeli wanaonung’unika. 28 Hivyo waambie, ‘Hakika kama niishivyo, asema Mwenyezi Mungu, nitawafanyia vitu vilevile nilivyosikia mkisema: 29 Kila mmoja wenu mwenye umri wa miaka ishirini au zaidi ambaye alihesabiwa na amenung’unika dhidi yangu, miili yenu itaanguka katika jangwa hili. 30 Hakuna hata mmoja wenu atakayeingia katika nchi niliyoapa kwa mkono ulioinuliwa kuwa makao yenu, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni. 31 Lakini watoto wenu ambao mlisema watachukuliwa mateka, nitawaingiza humo ili waifurahie nchi ambayo ninyi mmeikataa. 32 Bali ninyi, miili yenu itaanguka katika jangwa hili. 33 Watoto wenu watakuwa wachungaji wa mifugo hapa kwa miaka arobaini, wakiteseka kwa ajili ya kukosa uaminifu kwenu, hadi mwili wa mtu wenu wa mwisho ulale katika jangwa hili. 34 Kwa miaka arobaini, mwaka mmoja kwa kila siku katika zile siku arobaini mlizoipeleleza nchi, mtateseka kwa ajili ya dhambi zenu, na kujua jinsi ilivyo vibaya kunifanya mimi kuwa adui yenu.’ 35 Mimi Mwenyezi Mungu nimesema, na hakika nitafanya mambo haya kwa jumuiya hii yote ovu, ambayo imefungamana pamoja dhidi yangu. Watakutana na mwisho wao katika jangwa hili; hapa ndipo watafia.”
36 Hivyo watu wale ambao Musa alikuwa amewatuma kuipeleleza nchi, waliorudi na kuifanya jumuiya nzima kunung’unika dhidi ya Musa kwa kueneza taarifa mbaya kuhusu hiyo nchi: 37 watu hawa waliohusika kueneza taarifa mbaya kuhusu hiyo nchi walipigwa na kuanguka kwa tauni mbele za Mwenyezi Mungu. 38 Miongoni mwa watu walioenda kuipeleleza hiyo nchi, ni Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune peke yao waliosalia.
39 Musa alipotoa taarifa hii kwa Waisraeli wote, waliomboleza kwa uchungu. 40 Asubuhi na mapema siku iliyofuata, walipanda kilele kirefu cha nchi ya vilima, wakasema, “Tumetenda dhambi. Tutakwea hadi mahali Mwenyezi Mungu alipotuahidi.”
41 Lakini Musa akasema, “Kwa nini hamtii amri ya Mwenyezi Mungu? Jambo hili halitafanikiwa! 42 Msipande juu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu hayupo pamoja nanyi. Mtashindwa na adui zenu, 43 kwa kuwa Waamaleki na Wakanaani watapambana nanyi huko. Kwa sababu mmemwacha Mwenyezi Mungu, hatakuwa pamoja nanyi, ninyi mtaanguka kwa upanga.”
44 Hata hivyo, kwa kiburi chao walipanda juu kuelekea nchi ya vilima virefu, ijapokuwa Musa hakutoka kambini wala Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu. 45 Ndipo Waamaleki na Wakanaani walioishi katika hiyo nchi ya vilima wakateremka na kuwashambulia, wakawapiga njia yote hadi Horma.
* 14:25 yaani Bahari Nyekundu au Bahari ya Mafunjo