15
Sadaka za nyongeza
1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
2 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Baada ya ninyi kuingia katika nchi ninayowapa kama nyumbani,
3 nanyi mkitoa sadaka za kuteketezwa kwa moto, kutoka makundi ya ng’ombe au kondoo, kama harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu, ikiwa ni sadaka za kuteketezwa au dhabihu, kwa ajili ya nadhiri maalum ama sadaka ya hiari au sadaka ya sikukuu zenu,
4 ndipo yeye aletaye sadaka yake ataiweka mbele za Mwenyezi Mungu sadaka ya nafaka, sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta.
5 Pamoja na kila mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, andaa robo ya hini ya divai kwa sadaka ya kinywaji.
6 “ ‘Pamoja na kondoo dume, andaa sadaka ya nafaka ya sehemu mbili za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na theluthi moja ya hini ya mafuta,
7 na theluthi moja ya hini ya divai kuwa sadaka ya kinywaji. Vitoe kama harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu.
8 “ ‘Unapoandaa fahali mchanga kama sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, kwa ajili ya nadhiri maalum au sadaka ya amani kwa Mwenyezi Mungu,
9 leta pamoja na huyo fahali sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi ya efa uliochanganywa na nusu ya hini ya mafuta.
10 Pia utaleta nusu ya hini ya divai kuwa sadaka ya kinywaji. Itakuwa sadaka iliyoteketezwa kwa moto, harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu.
11 Kila fahali au kondoo dume, kila mwana-kondoo au mbuzi mchanga, atatayarishwa kwa njia hii.
12 Fanyeni hivi kwa ajili ya kila mmoja, kwa kadiri ya wingi wa mtakavyoandaa.
13 “ ‘Kila mmoja ambaye ni mzawa ni lazima afanye vitu hivi kwa njia hii hapo aletapo sadaka ya kuteketezwa kwa moto kama harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu.
14 Kwa vizazi vijavyo, wakati wowote mgeni au mtu mwingine yeyote anayeishi miongoni mwenu aletapo sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu, ni lazima afanye sawasawa kabisa na jinsi mnavyofanya ninyi.
15 Jumuiya itakuwa na sheria hizo hizo kwenu na kwa mgeni aishiye miongoni mwenu; hili ni agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. Ninyi na mgeni mtakuwa sawa mbele za Mwenyezi Mungu:
16 Sheria hizo na masharti hayo vitawahusu ninyi na pia mgeni aishiye miongoni mwenu.’ ”
17 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
18 “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi ninayowapeleka,
19 nanyi mkala chakula cha nchi hiyo, toeni sehemu ya chakula hicho kuwa sadaka kwa Mwenyezi Mungu.
20 Toeni andazi kutoka kwa malimbuko ya chakula chenu kitokacho katika ardhi, na mkitoe kama sadaka kutoka sakafu ya kupuria nafaka.
21 Kwa vizazi vyote vijavyo hamna budi kutoa sadaka hii kwa Mwenyezi Mungu kutoka kwa malimbuko ya unga wenu.
Sadaka kwa ajili ya dhambi isiyo ya makusudi
22 “ ‘Basi kama pasipo kukusudia umeshindwa kushika mojawapo katika amri hizi ambazo Mwenyezi Mungu alimpa Musa,
23 amri yoyote ya Mwenyezi Mungu kwenu kupitia Musa, tangu siku ile Mwenyezi Mungu alipowapa na inaendelea hadi vizazi vyote vijavyo;
24 ikiwa hili limefanyika pasipo kukusudia bila jumuiya kuwa na habari nalo, basi jumuiya yote itatoa fahali mchanga kuwa sadaka ya kuteketezwa ikiwa harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi Mungu, pamoja na sadaka ya nafaka na ya kinywaji zilizoamriwa kwayo, na beberu kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
25 Kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya jumuiya yote ya Waisraeli, nao watasamehewa, kwa kuwa haikuwa makusudi nao wamemletea Mwenyezi Mungu sadaka iliyoteketezwa kwa moto na sadaka ya dhambi kwa ajili ya kosa lao.
26 Jumuiya yote ya Waisraeli pamoja na wageni wanaoishi miongoni mwao watasamehewa, kwa sababu watu wote walihusika katika kosa lile lisilokusudiwa.
27 “ ‘Lakini kama mtu mmoja peke yake akitenda dhambi pasipo kukusudia, ni lazima alete mbuzi jike wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
28 Kuhani atafanya upatanisho mbele za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya yule aliyekosa kwa kufanya dhambi pasipo kukusudia, upatanisho utakapofanywa kwa ajili yake, atasamehewa.
29 Sheria hiyo moja itamhusu kila mmoja ambaye ametenda dhambi pasipo kukusudia, awe Mwisraeli mzawa ama mgeni.
30 “ ‘Lakini yeyote ambaye amefanya dhambi kwa dharau awe mzawa au mgeni, anamkufuru Mwenyezi Mungu, naye mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
31 Kwa sababu amelidharau neno la Mwenyezi Mungu na kuvunja amri zake, mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali; hatia yake inabaki juu yake.’ ”
Mvunja Sabato auawe
32 Waisraeli walipokuwa jangwani, mtu mmoja alikutwa akikusanya kuni siku ya Sabato.
33 Wale waliomkuta akikusanya kuni wakamleta kwa Musa, na Haruni na kusanyiko lote,
34 nao wakamweka kifungoni, kwa sababu haikufahamika kwa wazi kwamba afanyiwe nini.
35 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Huyo mtu ni lazima afe. Kusanyiko lote lazima wampige mawe nje ya kambi.”
36 Hivyo kusanyiko wakamtoa nje ya kambi na kumpiga mawe hadi akafa, kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.
Vifundo kwenye mavazi
37 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
38 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Kwa vizazi vyote vijavyo jifanyieni vifundo katika pindo za mavazi yenu vikiwa na uzi wa buluu kwenye kila kifundo.
39 Mtakuwa mkivitazama vifundo hivyo ili mpate kukumbuka amri zote za Mwenyezi Mungu, ili mpate kuzitii msije mkajitia uzinzi wenyewe kwa kuzifuata tamaa za mioyo yenu na za macho yenu.
40 Ndipo mtakumbuka kuzitii amri zangu zote nanyi mtawekwa wakfu kwa Mungu wenu.
41 Mimi Ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa Misri niwe Mungu wenu. Mimi Ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.’ ”