16
Kora, Dathani na Abiramu
1 Kora mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, pamoja na baadhi ya Wareubeni, yaani Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni mwana wa Pelethi, wakachukua baadhi ya watu,
2 wakainuka dhidi ya Musa. Pamoja nao walikuwa wanaume Waisraeli mia mbili na hamsini, watu waliojulikana, viongozi wa jumuiya waliokuwa wameteuliwa kuwa wakuu wa kusanyiko.
3 Wakaja kama kikundi kuwapinga Musa na Haruni, wakawaambia, “Ninyi mmejitukuza sana! Kusanyiko hili wote ni watakatifu, kila mmoja wao, naye Mwenyezi Mungu yu pamoja nao. Kwa nini basi mmejitukuza wenyewe juu ya kusanyiko la Mwenyezi Mungu?”
4 Musa aliposikia jambo hili, akaanguka kifudifudi.
5 Kisha akamwambia Kora na wafuasi wake wote: “Asubuhi Mwenyezi Mungu ataonesha ni nani aliye wake na ni nani aliye mtakatifu, tena atamtaka mtu huyo aje kwake. Mtu yule ambaye atamchagua atamfanya kuja karibu naye.
6 Wewe Kora na wafuasi wako wote mtafanya hivi: Chukueni vyetezo,
7 kesho wekeni moto na uvumba kwenye hivyo vyetezo mbele za Mwenyezi Mungu. Mtu ambaye Mwenyezi Mungu atamchagua atakuwa ndiye mtakatifu. Ninyi Walawi mmejitukuza sana!”
8 Pia Musa akamwambia Kora, “Enyi Walawi! Sasa nisikilizeni.
9 Haiwatoshi ninyi kwamba Mungu wa Israeli amewateua ninyi kutoka kusanyiko lote la Israeli, na kuwaleta karibu naye mpate kufanya kazi kwenye Maskani ya Mwenyezi Mungu, na kusimama mbele ya kusanyiko ili kuwahudumia?
10 Amekuleta wewe na ndugu zako Walawi mwe karibu naye; lakini sasa unajaribu kuchukua ukuhani pia.
11 Wewe na wafuasi wako wote mmekusanyika pamoja kinyume cha Mwenyezi Mungu. Haruni ni nani kwamba ninyi mnung’unike dhidi yake?”
12 Kisha Musa akawaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu. Lakini wao wakasema, “Sisi hatuji!
13 Haitoshi tu kwamba wewe umetuleta kutoka nchi inayotiririka maziwa na asali ili kutuua sisi jangwani? Nawe sasa pia unataka kuwa mkuu juu yetu?
14 Zaidi ya hayo, hujatuingiza katika nchi inayotiririka maziwa na asali, wala hujatupatia urithi wa mashamba na mashamba ya mizabibu. Je, utayang’oa macho ya watu hawa? Hapana, sisi hatuji!”
15 Ndipo Musa akakasirika sana na kumwambia Mwenyezi Mungu, “Usiikubali sadaka yao. Mimi sikuchukua chochote, hata punda kutoka kwao, wala sijamkosea hata mmoja wao.”
16 Musa akamwambia Kora, “Wewe na wafuasi wako wote kesho mtatokea mbele za Mwenyezi Mungu: wewe na hao wenzako, pamoja na Haruni.
17 Kila mtu atachukua chetezo chake na kuweka uvumba ndani, vyetezo mia mbili na hamsini kwa jumla, na kukileta mbele za Mwenyezi Mungu. Wewe na Haruni mtaleta vyetezo vyenu pia.”
18 Kwa hiyo kila mtu akachukua chetezo chake, akaweka moto na uvumba ndani, na kusimama pamoja na Musa na Haruni kwenye mlango wa Hema la Kukutania.
19 Kora alipokuwa amekusanya wafuasi wake wote kuwapinga Musa na Haruni kwenye mlango wa Hema la Kukutania, utukufu wa Mwenyezi Mungu ukatokea kwa kusanyiko lote.
20 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni,
21 “Jitengeni na kusanyiko hili ili nipate kuwaangamiza mara moja.”
22 Lakini Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi na kulia kwa sauti, wakasema, “Ee Mungu, Mungu wa roho za wanadamu wote, utakuwa na hasira na kusanyiko lote wakati ni mtu mmoja tu ametenda dhambi?”
23 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
24 “Waambie kusanyiko, ‘Ondokeni hapo karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu.’ ”
25 Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu, nao wazee wa Israeli wakafuatana naye.
26 Musa akawaonya kusanyiko, “Sogeeni nyuma mbali na mahema ya hawa watu waovu! Msiguse kitu chochote kilicho mali yao, la sivyo mtafagiliwa mbali kwa sababu ya dhambi zao zote.”
27 Hivyo wakaondoka karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu. Dathani na Abiramu walikuwa wametoka nje, nao walikuwa wamesimama pamoja na wake zao, watoto wao na wale wanyonyao kwenye mlango wa mahema yao.
28 Ndipo Musa akasema, “Hivi ndivyo mtakavyojua kuwa Mwenyezi Mungu amenituma kufanya mambo haya, na kwamba halikuwa wazo langu.
29 Ikiwa watu hawa watakufa kifo cha kawaida na kupatwa na yale ya kawaida yanayowapata wanadamu, basi Mwenyezi Mungu hakunituma mimi.
30 Lakini ikiwa Mwenyezi Mungu ataleta jambo jipya kabisa, ardhi ikifunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na kila kitu kilicho mali yao, nao washuke chini kaburini wakiwa hai, ndipo mtafahamu kuwa watu hawa wamemdharau Mwenyezi Mungu.”
31 Mara Musa alipomaliza kusema haya yote, ardhi iliyokuwa chini yao ikapasuka,
32 nchi ikafunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na jamaa zao, na watu wote wa Kora na mali yao yote.
33 Wakashuka chini kaburini wakiwa hai, pamoja na kila kitu walichokuwa nacho; nchi ikajifunika juu yao, nao wakaangamia wakatoweka kutoka kwa kusanyiko.
34 Kutoka kilio chao, Waisraeli wote waliowazunguka walikimbia, wakipaza sauti, “Nchi inatumeza na sisi pia!”
35 Moto ukaja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ukawateketeza wale watu mia mbili na hamsini waliokuwa wakifukiza uvumba.
36 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
37 “Mwambie Eleazari mwana wa kuhani Haruni, atoe vyetezo kwenye mabaki ya moto na kutawanya makaa mbali kiasi, kwa maana vyetezo ni vitakatifu:
38 vyetezo vya watu waliofanya dhambi iliyowagharimu maisha yao. Fua vyetezo hivyo kuwa bamba ili kufunika madhabahu, kwa maana vimeletwa mbele za Mwenyezi Mungu na vimekuwa vitakatifu. Navyo viwe ishara kwa Waisraeli.”
39 Hivyo kuhani Eleazari akavikusanya vile vyetezo vya shaba vilivyoletwa na wale waliokuwa wameteketezwa kwa moto, naye akavifua kufunika madhabahu,
40 kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwelekeza kupitia Musa. Hili lilikuwa kuwakumbusha Waisraeli kwamba hakuna mtu hata mmoja, isipokuwa mzao wa Haruni, awezaye kuja kufukiza uvumba mbele za Mwenyezi Mungu, la sivyo, angekuwa kama Kora na wafuasi wake.
41 Siku iliyofuata jumuiya yote ya Waisraeli wakanung’unika dhidi ya Musa na Haruni, wakisema, “Mmewaua watu wa Mwenyezi Mungu.”
42 Lakini kusanyiko walipokusanyika kupingana na Musa na Haruni, nao wakageuka kuelekea Hema la Kukutania, ghafula wingu likafunika Hema, nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukatokea.
43 Ndipo Musa na Haruni wakaenda mbele ya Hema la Kukutania,
44 naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,
45 “Jitenge mbali na kusanyiko hili ili niweze kuwaangamiza mara moja.” Wakaanguka kifudifudi.
46 Kisha Musa akamwambia Haruni, “Chukua chetezo chako na uweke uvumba ndani, pamoja na moto kutoka madhabahuni, nawe uende haraka kwenye kusanyiko ili kufanya upatanisho kwa ajili yao. Ghadhabu imekuja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na tauni imeanza.”
47 Hivyo Haruni akafanya kama Musa alivyosema, akakimbilia katikati ya kusanyiko. Tauni ilikuwa tayari imeanza miongoni mwa watu, lakini Haruni akafukiza uvumba na kufanya upatanisho kwa ajili yao.
48 Haruni akasimama kati ya waliokuwa hai na waliokufa, nayo tauni ikakoma.
49 Lakini walikufa watu elfu kumi na nne na mia saba kutokana na tauni hiyo, licha ya wale waliokuwa wamekufa kwa sababu ya Kora.
50 Ndipo Haruni akamrudia Musa kwenye mlango wa Hema la Kukutania, kwa maana tauni ilikuwa imekoma.