23
Uasi dhidi ya Athalia
(2 Wafalme 11:4-20)
Katika mwaka wa saba, Yehoyada akaonesha nguvu zake. Alifanya agano na wakuu wa vikosi vya mamia: yaani Azaria mwana wa Yerohamu, Ishmaeli mwana wa Yehohanani, Azaria mwana wa Obedi, Maaseya mwana wa Adaya, na Elishafati mwana wa Zikri. Wakazunguka katika Yuda yote na kukusanya Walawi na viongozi wa jamaa za Israeli kutoka miji yote. Walipofika Yerusalemu, kusanyiko lote wakafanya agano na mfalme katika Hekalu la Mungu.
Yehoyada akawaambia, “Mwana wa mfalme atatawala, kama Mwenyezi Mungu alivyoahidi kuhusu wazao wa Daudi. Basi hivi ndivyo iwapasavyo kufanya: Theluthi yenu makuhani na Walawi ambao mnaingia zamu siku ya Sabato mtalinda milangoni, theluthi yenu mtalinda jumba la kifalme, na theluthi nyingine mtalinda Lango la Msingi. Walinzi wengine wote mwe ndani ya nyua za Hekalu la Mwenyezi Mungu. Hakuna mtu yeyote ataingia katika Hekalu la Mwenyezi Mungu isipokuwa makuhani na Walawi walio kwenye zamu. Wao wanaweza kuingia kwa sababu ni watakatifu, lakini watu wengine wote itawapasa kulinda kile walichoamriwa na Mwenyezi Mungu. Walawi watajipanga kumzunguka mfalme, kila mtu akiwa na silaha zake mkononi. Mtu mwingine yeyote aingiaye Hekaluni lazima auawe. Kaeni karibu na mfalme popote aendapo.”
Walawi na watu wote wa Yuda wakafanya vile kuhani Yehoyada aliagiza. Kila mmoja akawachukua watu wake, wale waliokuwa wakiingia zamu siku ya Sabato na wale waliokuwa wakienda mapumziko, kwa sababu kuhani Yehoyada hakuruhusu kikosi chochote kiondoke. Kisha kuhani Yehoyada akawapa wakuu wa vikosi vya mamia mikuki na ngao kubwa na ndogo zilizokuwa za Mfalme Daudi, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mungu. 10 Akawapanga walinzi wote kumzunguka mfalme, kila mmoja akiwa na silaha yake mkononi mwake, karibu na madhabahu na Hekalu, kuanzia upande wa kusini hadi upande wa kaskazini mwa Hekalu.
11 Yehoyada na wanawe wakamtoa Yoashi mwana wa mfalme nje na kumvika taji. Wakampa nakala ya agano na kumtangaza kuwa mfalme. Wakampaka mafuta na kupaza sauti, wakisema, “Mfalme aishi maisha marefu!”
12 Athalia aliposikia kelele za watu wakikimbia na kumsifu mfalme, akawaendea watu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. 13 Akaangalia, na tazama, mfalme alikuwa amesimama karibu na nguzo yake kwenye ingilio. Maafisa na wapiga tarumbeta walikuwa kando ya mfalme, nao watu wote wa nchi walikuwa wanashangilia na kupiga tarumbeta, na waimbaji waliokuwa na vyombo vya uimbaji walikuwa wakiongoza nyimbo za sifa. Ndipo Athalia akararua mavazi yake na kulia, “Uhaini! Uhaini!”
14 Kuhani Yehoyada akawatuma majemadari wa vikosi vya mamia, waliokuwa viongozi wa jeshi, na kuwaambia: “Mleteni nje kati ya safu, na mkamuue kwa upanga yeyote anayemfuata.” Kwa kuwa kuhani alikuwa amesema, “Msimuulie ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.” 15 Kwa hiyo wakamkamata alipofika kwenye ingilio la Lango la Farasi, katika viwanja vya jumba la mfalme, wakamuua hapo.
16 Kisha Yehoyada akafanya agano kwamba yeye na watu wote na mfalme watakuwa watu wa Mwenyezi Mungu. 17 Watu wote wakaenda kwenye hekalu la Baali na kulibomoa. Wakavunjavunja madhabahu pamoja na sanamu, na kumuua Matani kuhani wa Baali mbele ya hayo madhabahu.
18 Yehoyada akaweka uangalizi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu mikononi mwa makuhani, hao Walawi, ambao Mfalme Daudi alikuwa amewagawa ili wahudumu hekaluni kwa ajili ya kutoa sadaka za kuteketezwa za Mwenyezi Mungu, kama ilivyoandikwa katika Torati ya Musa, kwa kushangilia na kuimba, vile Daudi alikuwa ameagiza. 19 Pia akawaweka mabawabu kwenye malango ya Hekalu la Mwenyezi Mungu ili kwa vyovyote asije akaingia mtu yeyote aliye najisi.
20 Akawachukua majemadari wa mamia, watu waheshimiwa, viongozi wa watu pamoja na watu wote wa nchi na kumteremsha mfalme kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu. Wakaingia kwenye jumba la mfalme kupitia Lango la Juu na kumkalisha mfalme kwenye kiti cha ufalme; 21 nao watu wote wa nchi wakafurahi. Mji ukatulia kwa sababu Athalia alikuwa ameuawa kwa upanga.