24
Yoashi akarabati Hekalu
(2 Wafalme 12:1-16)
Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka arobaini. Mama yake aliitwa Sibia aliyekuwa ametoka Beer-Sheba. Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu miaka yote ya Yehoyada kuhani. Yehoyada akamwoza wake wawili, akazaa watoto wa kiume na wa kike.
Baada ya muda, Yoashi akaamua kukarabati Hekalu la Mwenyezi Mungu. Akawaita pamoja makuhani na Walawi akawaambia, “Nendeni katika miji ya Yuda mkakusanye fedha wanazopaswa kulipa kila mwaka kutoka kwa Israeli wote, ili kukarabati Hekalu la Mungu wenu. Fanyeni hivyo sasa.” Lakini Walawi hawakufanya upesi.
Kwa hiyo mfalme akamwita Yehoyada kuhani mkuu na kumwambia, “Kwa nini hukuwaambia Walawi walete kutoka Yuda na Yerusalemu kodi iliyowekwa na Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu pamoja na kusanyiko la Israeli kwa ajili ya Hema la Ushuhuda?”
Kwa kuwa wana wa yule mwanamke mwovu Athalia, walikuwa wamevunja na kuingia katika Hekalu la Mungu, nao wakawa wamevitumia hata vile vitu vilivyowekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu kwa mabaali.
Kwa amri ya mfalme, likatengenezwa kasha, nalo likawekwa nje kwenye lango la Hekalu la Mwenyezi Mungu. Tangazo likatolewa katika Yuda na Yerusalemu, kwamba inapasa wamletee Mwenyezi Mungu kodi ambayo Musa, mtumishi wa Mwenyezi Mungu, alikuwa amewaagiza Israeli huko jangwani. 10 Maafisa wote na watu wote wakaleta michango yao kwa furaha, wakaweka kwenye kasha hadi likajaa. 11 Ikawa kila wakati kasha lilipoletwa ndani na Walawi kwa maafisa wa mfalme na kuona kwamba kuna kiasi kikubwa cha fedha, mwandishi wa mfalme na afisa wa kuhani mkuu walikuwa wanakuja na kumimina, kisha kulirudisha mahali pake. Walifanya hivi mara kwa mara, nao wakakusanya fedha nyingi sana. 12 Mfalme na Yehoyada wakawapa wale watu waliofanya kazi iliyotakiwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Wakawaajiri waashi na maseremala ili kutengeneza Hekalu la Mwenyezi Mungu, pia wafanyakazi za chuma na shaba ili kukarabati Hekalu la Mwenyezi Mungu.
13 Watu walioshughulika na kazi walikuwa wenye bidii, nayo kazi ya kukarabati ikaendelea vizuri mikononi mwao. Wakalitengeneza upya Hekalu la Mwenyezi Mungu likarudi katika hali yake ya awali, na wakaliimarisha. 14 Walipokamilisha kazi hiyo ya kukarabati, wakaleta fedha zilizobaki wakampa mfalme na Yehoyada, nao kwa hizo wakatengeneza vyombo kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu: Vyombo kwa ajili ya huduma na kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia mabakuli na vitu vingine vya dhahabu na fedha. Wakati wote Yehoyada akiwa hai, sadaka za kuteketezwa zilitolewa wakati wote katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
15 Basi Yehoyada alikuwa mzee aliyeshiba siku alipofariki. Alikufa akiwa na umri wa miaka mia moja na thelathini. 16 Wakamzika pamoja na wafalme katika Mji wa Daudi, kwa sababu ya mema aliyokuwa ametenda katika Israeli kwa ajili ya Mungu na Hekalu lake.
Uovu wa Yoashi
17 Baada ya kifo cha Yehoyada, wakuu wa Yuda walikuja kumpa mfalme heshima, naye akawasikiliza. 18 Wakaacha Hekalu la Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, wakaabudu nguzo za maashera na sanamu. Kwa sababu ya hatia yao, hasira ya Mungu ikawajia Yuda na Yerusalemu. 19 Ingawa Mwenyezi Mungu aliwatuma manabii wawarudishe watu kwake na ingawa waliwaonya, hawakuwasikiliza.
20 Ndipo Roho wa Mwenyezi Mungu akaja juu ya Zekaria mwana wa Yehoyada kuhani. Akasimama mbele ya watu akasema, “Hili ndilo asemalo Mungu, ‘Kwa nini mnakataa kuzitii amri za Mwenyezi Mungu? Hamtafanikiwa kwa kuwa mmemwacha Mwenyezi Mungu, naye amewaacha ninyi.’ ”
21 Lakini wakapanga njama dhidi yake, na kwa amri ya mfalme wakampiga kwa mawe hadi akafa katika ua wa Hekalu la Mwenyezi Mungu. 22 Mfalme Yoashi hakukumbuka wema aliotendewa na Yehoyada baba yake Zekaria, ila alimuua mwanawe, ambaye alisema wakati akiwa amelala akingojea kufa, “Mwenyezi Mungu na alione hili na alipize kisasi.”
23 Mwishoni mwa ule mwaka, jeshi la Waaramu likaja dhidi ya Yoashi, likavamia Yuda na Yerusalemu na kuwaua viongozi wote wa watu. Wakapeleka nyara zao zote kwa mfalme wao huko Dameski. 24 Ingawa jeshi la Waaramu lilikuwa limekuja na watu wachache tu, Mwenyezi Mungu akatia mikononi mwao jeshi kubwa kuliko lao. Kwa sababu Yuda walikuwa wamemwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, hukumu ilitekelezwa juu ya Yoashi. 25 Waaramu walipoondoka, walimwacha Yoashi akiwa mgonjwa sana. Maafisa wake wakapanga njama dhidi yake kwa sababu alikuwa amemuua mwana wa Kuhani Yehoyada, nao wakamuua kitandani mwake. Hivyo akafa, wakamzika katika Mji wa Daudi, lakini si katika makaburi ya wafalme.
26 Wale waliopanga njama dhidi yake walikuwa Zabadi mwana wa Shimeathi mwanamke Mwamoni, na Yehozabadi mwana wa Shimrithi mwanamke Mmoabu. 27 Kwa habari za wanawe, unabii mwingi kumhusu na kumbukumbu za kutengenezwa upya kwa Hekalu la Mungu, zimeandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme. Amazia mwanawe akawa mfalme baada yake.