12
1 Kuhusu karama za rohoni, kaka na dada zangu sitaki mkose kufahamu.
2 Mwajua ya kuwa mlipokuwa wapagani mliongozwa kufuata sanamu zisizoongea, kwa njia zozote mliongozwa nazo.
3 Kwa hiyo, nataka mfahamu kwamba hakuna yeyote anenaye kwa Roho wa Mungu akisema, “Yesu amelaaniwa.” Hakuna yeyote atakayesema, “Yesu ni Bwana,” isipokuwa katika Roho Mtakatifu.
4 Basi kuna karama tofauti tofauti, bali Roho ni yeye yule.
5 Na kuna huduma tofauti tofauti, bali Bwana ni yeye yule.
6 Na kuna aina mbalimbali za kazi, lakini Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.
7 Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote.
8 Maana mtu mmoja amepewa na Roho neno la hekima, na mwingine neno la maarifa kwa Roho yule yule.
9 Kwa mwingine humpa imani kwa Roho yeye yule, na kwa mwingine karama ya uponyaji kwa Roho mmoja.
10 Kwa mwingine matendo ya nguvu, na mwingine unabii. Na kwa mwingine uwezo wa kupambanua roho, mwingine aina mbalimbali za lugha, na kwa mwingnine tafsiri za lugha.
11 Lakini Roho ni yule yule atendaye kazi hizi zote, kumpa kila mtu karama kwa kadiri ya uchaguzi wake mwenyewe.
12 Kwa maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote ni vya mwili ule ule, vivyo hivyo na Kristo.
13 Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi au Wayunani, kwamba tu watumwa au huru, na wote tulinyweshwa Roho mmoja.
14 Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi.
15 Ikiwa mguu utasema, “kwa kuwa mimi si mkono, mimi si sehemu ya mwili,” hiyo haiufanyi kutokuwa sehemu ya mwili.
16 Na ikiwa sikio litasema, “kwa kuwa mimi si jicho, mimi si sehemu ya mwili,” hiyo hailifanyi kutokuwa sehemu ya mwili.
17 Kama mwili wote utakuwa jicho, kungekuwa wapi kusikia? Kama mwili wote ukiwa sikio, kungekuwa wapi kunusa?
18 Lakini Mungu aliweka kila kiungo cha mwili mahali pake kama alivyopanga mwenyewe.
19 Na kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?
20 Hivyo sasa viungo ni vingi, lakini mwili ni mmoja.
21 Jicho haliwezi kuuambia mkono, “sina haja na wewe.” Wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu, sina haja na ninyi.”
22 Lakini viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa na heshima kidogo vyahitajika zaidi.
23 Na viungo vya mwili tunavyodhani vina heshima kidogo, twavipa heshima zaidi, na viungo vyetu visivyo na mvuto vina uzuri zaidi.
24 Na sasa viungo vyetu vilivyo na mvuto havina haja ya kupewa heshima, kwa kuwa tayari vina heshima. Lakini Mungu ameviunganisha viungo vyote pamoja, na amevipa heshima zaidi vile visivyo heshimiwa.
25 Alifanya hivyo ili pasiwepo mgawanyiko katika mwili, bali viungo vyote vitunzane kwa upendo wa mmoja.
26 Na wakati kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote vyaumia kwa pamoja. Au wakati kiungo kimoja kikiheshimiwa, viungo vyote vifurahi kwa pamoja.
27 Sasa ninyi ni mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake.
28 Na Mungu ameweka katika kanisa kwanza mitume, pili manabii, tatu waalimu, kisha wale wote watendao matendo makuu, kisha karama za uponyaji, wale wasaidiao, wale wafanyao kazi ya kuongoza, na wote walio na aina mbalimbali za lugha.
29 Je sisi sote ni mitume? Sisi sote ni manabii? Sisi sote ni waalimu? Je sisi sote tunafanya matendo ya miujiza?
30 Je sisi sote tuna karama ya uponyaji? Sisi sote tunaongea kwa lugha? Sisi sote tunatafsiri lugha?
31 Tafuteni sana karama zilizo kuu. Nami nitawaonesha njia iliyo bora zaidi.