13
1 Tuseme kwamba ninanena kwa lugha za wanadamu na za malaika. Lakini kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo au upatu uvumao.
2 Na kwamba nina karama ya unabii na ufahamu wa kweli zilizofichika na maarifa, na kwamba ninayo imani ya kuhamisha milima. Lakini ikiwa sina upendo, mimi si kitu.
3 Na tuseme kwamba ninatoa milki yangu yote na kuwalisha masikini, na kwamba ninautoa mwili wangu ili nichomwe moto. Lakini kama sina upendo, hainifaidii kitu.
4 Upendo huvumilia na hufadhili. Upendo haujisifu au kujivuna. Hauna kiburi
5 au ukorofi. Hautafuti mambo yake, hauoni uchungu haraka, wala hauhesabu mabaya.
6 Haufurahii udhalimu. Badala yake, hufurahi katika kweli.
7 Upendo huvumilia mambo yote; huamini mambo yote, una ujasiri katika mambo yote, na hustahimili mambo yote.
8 Upendo haukomi. Ikiwa kuna unabii, wote utapita. Ikiwa kuna lugha, zitakoma. Ikiwa kuna maarifa, yatapita.
9 Kwa kuwa tunajua kwa sehemu na tunafanya unabii kwa sehemu.
10 Lakini ijapo ile iliyo kamili, ile isiyo kamili itapita.
11 Nilipokuwa mtoto, nilisema kama mtoto, nilifikiri kama mtoto, niliamua kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima, niliweka mbali nami mambo ya kitoto.
12 Kwa kuwa sasa tunaona kama kwa kioo, kama sura gizani, lakini wakati ule tutaona uso kwa uso. Sasa ninajua kwa sehemu, lakini wakati ule nitajua sana kama na mimi ninavyojulikana sana.
13 Lakini sasa mambo haya matatu yanadumu: imani, tumaini lijalo, na upendo. Lakini lililo kuu zaidi ya haya ni upendo.