1 Wathesalonike
1
1 Paulo, Silwano na Timotheo kwa kanisa la Wathesalonike katika Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo. Neema na amani iwe nanyi.
2 Tunatoa shukrani kwa Mungu kila mara kwa ajili yenu nyote, wakati tunapowataja katika maombi yetu.
3 Tunaikumbuka bila kukoma mbele ya Mungu na baba yetu kazi yenu ya imani, juhudi ya upendo, na uvumilivu wenye ujasiri kwa ajili ya baadaye katika Bwana Yesu Kristo.
4 Ndugu Mnaopendwa na Mungu, tunajua wito wenu.
5 Na jinsi injili yetu ilivyokuja kwenu si kwa neno tu, bali pia katika nguvu, katika Roho Mtakatifu, na katika uhakika. Kwa namna hiyo, mnajua pia sisi tulikuwa watu wa namna gani miongoni mwenu kwa ajili yenu.
6 Mlikuwa watu wa kutuiga sisi na Bwana, kama mlivyopokea neno katika taabu kwa furaha itokayo kwa Roho Mtakatifu.
7 Na matokeo yake, mkawa mfano kwa wote katika Makedonia na Akaiya ambao wanaamini.
8 Kwa kuwa kutoka kwenu neno la Mungu limeenea kote, na si kwa Mekadonia na Akaiya peke yake. Badala yake, kwa kila mahali imani yenu katika Mungu imeenea kote. Na matokeo yake, hatuhitaji kusema chochote.
9 Kwa kuwa wao wenyewe wanaarifu ujio wetu ulikuwa wa namna gani kati yenu. Wanasimulia jinsi mulivyomgeukia Mungu kutoka katika sanamu na kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli.
10 Walitoa habari kuwa mnamsubiri Mwana wake kutoka mbinguni, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu. Na huyu ni Yesu, anayetuweka huru kutoka kwenye ghadhabu ijayo.