16
1 Nimewaambia mambo haya ili msiweze kukwazwa.
2 Watawatoa nje ya masinagogi; hakika saa inakuja ambayo kila atakayewaua atafikiri kuwa anafanya kazi njema kwa ajili ya Mungu.
3 Watawatendea mambo haya kwa sababu hawamfahamu Baba wala hawanifahamu mimi.
4 Nimewaambia mambo haya ili kwamba wakati ukifika wa haya kutokea, mnaweza kuyakumbuka na jinsi nilivyowaambia muweze wao. Sikuwaambia kuhusu mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi.
5 Japokuwa, sasa naenda kwa yule aliyenituma; lakini hakuna kati yenu anayeniuliza, “Unaenda wapi?”
6 Kwa sababu nimesema maneno haya kwenu, huzuni imejaa mioyoni mwenu.
7 Hata hivyo, nawaambia ukweli: ni vyema kwenu nikiondoka; kwa maana nisipoondoka, mfariji hatakuja kwen; lakini nikienda ntamtuma kwenu.
8 Akija, huyo mfariji ataubitisha ulimwengu kuhusiana na dhambi, kuhusiana na haki na kuhusiana na hukumu.
9 Kuhusiana na dhambi, kwa sababu hawakuniamini mimi,
10 kuhusiana na haki, kwa sababu naenda kwa baba, na hamtaniona tena;
11 na kuhusiana na hukumu kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amehukumiwa.
12 Ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamtayaelewa sasa.
13 Lakini, yeye, Roho wa kweli, akija, atawaongoza katika kweli yote; kwa kuwa hataongea kwa ajili yake mwenyewe; lakini yoyote atakayoyasikia, atayasema mambo hayo; na atayadhihirisha kwenu mambo yatakayokuja.
14 Yeye atanitukuza mimi, kwa sababu atayachukua mambo yangu na atayatangaza kwenu.
15 Vitu vyote alivyonavyo Baba ni vyangu; kwa hiyo, nimesema kwamba Roho atachukua mambo yangu na atayadhihirisha kwenu.
16 Bado muda mfupi, hamtaniona tena; na baada ya muda mfupi tena, mtaniona.”
17 Baadhi ya wanafunzi wake wakaambizana, “Ni nini anachotuambia, “muda mfupi, na hamtaniona tena,' na, kisha, mda mfupi mtaniona,' na, 'kwa sababu naenda kwa Baba?”
18 Kwa hiyo wakasema, “Ni kitu gani anachosema, 'Bado mda mfupi'? Hatujui asemavyo.”
19 Yesu aliona kuwa walitamani kumuuliza, naye akawaambia, “Mnajiuliza wenyewe kuhusu hili, nilivyosema, 'Bado muda mfupi, hamtaniona tena; na baada ya muda mfupi mtaniona'?
20 Amin, amin, nawaambia, mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utashangilia, mtakuwa na huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
21 Mwanamke anakuwa na huzuni wakati anapokuwa na uchungu kwa sababu wakati wa kujifungua umefika; lakini anapojifungua mtoto, hakumbuki tena maumivu kwa sababu ya furaha yake kwamba mtoto amezaliwa duniani.
22 Ninyi pia mna huzuni sasa, lakini nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi na hakuna atakayeweza kuiondoa furaha yenu.
23 Siku hiyo hamtaniuliza maswali. Amin, Amin, nawaambia, Mkiomba lolote kwa Baba, atawapa kwa jina langu.
24 Mpaka sasa hamjaomba lolote kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapokea ili kwamba furaha yenu ikamilike.
25 Nimezungumza na ninyi kwa lugha isiyoeleweka, lakini saa inakuja ambapo sitazungumza kwa lugha isiyoeleweka lakini badala yake nitawaambia waziwazi kuhusu Baba.
26 Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba nitaomba kwa Baba kwa ajili yenu;
27 Kwa kuwa Baba mwenyewe anawapenda kwa sababu mmenipenda mimi na kwa sababu mmeniamini kuwa nimetoka kwa Baba.
28 Nilitoka kwa Baba na nimekuja ulimwenguni; tena, naondoka ulimwenguni na ninaenda kwa Baba”.
29 Wanafunzi wake wakamwambia, “Unaona, sasa unaongea wazi wazi na hautumii mafumbo.
30 Sasa, tunajua kwamba unajua mambo yote, na hauhitaji mtu yoyote akuulize maswali. Kwa sababu hii tunaamini kuwa unatoka kwa Mungu.
31 Yesu akawajibu, “Sasa mmeamini?”
32 Tazama, saa inakuja, ndiyo na hakika imefika, ambapo mtatawanyika kila mmoja na kwa wa kwao mtaniacha mwenyewe. Lakini siko peke yangu kwa sababu Baba yupo nami.
33 Nawaambia mambo haya ili kwamba ndani yangu muwe na amani. Duniani mna matatizo, lakini jipeni moyo, nimeushinda ulimwengu.