5
1 Walikuja mpaka upande mwingine wa bahari, katika mkoa wa Gerasi
2 Na ghafla wakati Yesu alipokuwa akitoka nje ya mtumbwi, mtu mwenye roho chafu alikuja kwake kutoka makaburini.
3 Mtu huyu aliishi makaburini. Hakuna aliyeweza kumzuia zaidi, hakuna hata kwa minyororo.
4 Alikuwa amefungwa nyakati nyingi kwa pingu na minyororo. Aliikata minyororo na pingu zake zilivunjwa. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na nguvu za kumshinda.
5 Usiku na mchana akiwa makaburini na milimani, alilia na kujikata yeye mwenyewe kwa mawe makali.
6 Alipomwona Yesu kwa mbali, alikimbilia kwake na kuinama mbele yake.
7 Alilia kwa sauti kuu, “Wataka nikufanyie nini, Yesu, Mwana wa Mungu aliye Juu sana? Ninakusihi kwa Mungu mwenyewe, usinitese.”
8 Kwa kuwa alikuwa amemwambia, “Mtoke mtu huyu, wewe roho mchafu.”
9 Naye alimwuliza, “Jina lako ni nani?” Naye alimjibu, “Jina langu ni Legion, kwa kuwa tuko wengi.”
10 Alimsihi tena na tena asiwapeleke nje ya mkoa.
11 Sasa kundi kubwa la nguruwe lilikuwa likilishwa juu ya kilima,
12 nao walimsihi, wakisema, “Tutume kwa nguruwe; tuingie ndani yao.”
13 Hivyo aliwaruhusu; roho wachafu waliwatoka na kuingia ndani ya nguruwe, nao walikimbilia chini ya kilima mpaka baharini, na karibia nguruwe elfu mbili walizama baharini.
14 Na wale waliokuwa wakiwalisha nguruwe walikimbia na kutoa taarifa ya kilichotokea katika mji na katika nchi. Ndipo watu wengi walitoka kwenda kuona kilichotokea.
15 Ndipo walikuja kwa Yesu na walimwona mtu aliyepagawa na pepo—aliyekuwa na Jeshi—amekaa chini, amevikwa, na akiwa katika akili yake timamu, nao waliogopa.
16 Wale waliokuwa wameona kilichotokea kwa mtu aliyekuwa amepagawa na pepo waliwaambia kilichotokea kwake na pia kuhusu nguruwe.
17 Nao walianza kumsihi aondoke katika mkoa wao.
18 Na alipokuwa akiingia ndani ya mtumbwi, mtu aliyekuwa amepagawa na mapepo alimsihi kwamba aende pamoja naye.
19 Lakini hakumruhusu, lakini alimwambia, “Nenda nyumbani kwako na kwa watu wako, na uwaambie alikufanyia Bwana, na rehema aliyokupa.”
20 Hivyo alienda na alianza kutangaza mambo makuu ambayo Yesu amefanya kwake katika Dekapoli, na kila mmoja alistaajabu.
21 Na wakati Yesu alipovuka tena upande mwingine, ndani ya mtumbwi, umati mkubwa ulikusanyika kumzunguka, alipokuwa kando ya bahari.
22 Na mmoja wa kiongozi wa sinagogi, aliyeitwa Yairo, alikuja, na alipomwona, alianguka miguuni pake.
23 Akamsihi zaidi na zaidi, akisema, “ Binti yangu mdogo anakaribia kufa. Ninakusihi, njoo na uweke mikono yako juu yake ili kwamba aweze kupata afya na kuishi.”
24 Hivyo alikwenda pamoja naye, na umati mkubwa ulimfuata nao walimzonga karibu wakimzunguka.
25 Kulikuwa na mwanamke ambaye damu yake ilikuwa imetoka kwa miaka kumi na miwili.
26 Aliteseka vya kutosha chini ya matabibu wengi na alitumia kila kitu alichokuwa nacho. Hata hivyo hakusaidika kwa chochote, lakini badala yake alizidi kuwa na hali mbaya.
27 Alisikia habari kuhusu Yesu. Hivyo alikuja nyuma yake wakati alipokuwa akitembea ndani ya umati, naye aliligusa vazi lake.
28 Kwa kuwa alisema, “Kama nikiyagusa mavazi yake tu, nitakuwa mzima.”
29 Alipomgusa, kutokwa damu kulikoma, na alijisikia katika mwili wake kwamba aliponywa kutoka kwenye mateso yake.
30 Na ghafla Yesu aligundua ndani yake mwenyewe kwamba nguvu zimemtoka. Na aligeuka huku na huku katika umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyeligusa vazi langu?”
31 Wanafunzi wake walimwambia, “Unaona umati huu umekusonga ukikuzunguka, nawe wasema, 'Ni nani aliyenigusa?'”
32 Lakini Yesu alitazama huku na huku kuona ambaye aliyekuwa amefanya hili.
33 Mwanamke, akijua kilichotokea kwake, aliogopa na kutetemeka. Alikuja na alianguka chini mbele yake na kumwambia ukweli wote.
34 Alisema kwake, “Binti, imani yako imekufanya uwe mzima. Enenda kwa amani na uponywe kutoka kwenye ugonjwa wako.”
35 Alipokuwa akizungumza, baadhi ya watu walikuja kutoka kwa kiongozi wa Sinagogi, wakisema, “Binti yako amekufa. Kwa nini kuendelea kumsumbua mwalimu?”
36 Lakini Yesu aliposikia ambacho walikisema, alimwambia kiongozi wa Sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”
37 Hakumruhusu yeyote kuongozana naye, isipokuwa Petro, Yakobo, na Yohana, ndugu yake Yakobo.
38 Walikuja nyumbani kwa kiongozi wa Sinagogi naye aliona vurugu, kulia kwingi na kuomboleza.
39 Alipoingia nyumbani, aliwaambia, “Kwa nini mmesikitika na kwa nini mnalia? Mtoto hajafa bali amelala.”
40 Walimcheka, lakini yeye, aliwatoa wote nje, alimchukua baba wa mtoto na mama na wale waliokuwa pamoja naye, na aliingia ndani alimokuwa mtoto.
41 Aliuchukua mkono wa mtoto na alimwambia, “Talitha koum,” ambayo ni kusema, “Binti mdogo, nakuambia, amka.”
42 Ghafla mtoto aliamka na kutembea (kwa kuwa alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili). Na ghafla walishikwa na mshangao mkubwa.
43 Aliwaamuru kwa nguvu kwamba hakuna yeyote anapaswa kujua kuhusu hili. Na aliwaambia wampatie yule binti chakula.