6
1 Na akaondoka hapo na kwenda mjini kwao, na wanafunzi wake wakamfuata.
2 Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika Sinagogi. Watu wengi walimsikia na wakashangazwa. Wakasema, “Amepata wapi mafundisho haya?” “Ni hekima gani hii aliyopewa?” “Anatendaje miujiza hii kwa mikono yake?”
3 “Je huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu na ndugu yao kina Yakobo, Yose, Yuda na Simioni? Je dada zake si wanaishi papa hapa pamoja nasi?” Na hawakufurahishwa na Yesu.
4 Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika mji wake na miongoni mwa ndugu zake na nyumbani mwake.”
5 Hakuweza kutenda miujiza hapo, ila aliwawekea mikono wagonjwa wachache akawaponya.
6 Alishangazwa sana kwa sababu ya kutokuamini kwao. Kisha alivitembelea vijiji vya jirani akifundisha.
7 Aliwaita wale wanafunzi kumi na wawili akaanza kuwatuma wawili wawili. Aliwapa mamlaka juu ya pepo wachafu,
8 na kuwaamuru wasichukue chochote wanapokwenda isipokuwa fimbo tu. Wasichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kibindoni;
9 lakini wavae viatu, na siyo kanzu mbili.
10 Na akawaambia, “Nyumba yoyote mtakayoingia, kaeni hapo mpaka mtakapoondoka.
11 Na mji wowote usipowapokea wala kuwasikiliza, ondokeni kwao, kung'uteni mavumbi ya miguu yenu, iwe ushuhuda kwao.”
12 Nao wakaenda wakitangaza watu watubu na kuacha dhambi zao.
13 Waliwafukuza pepo wengi, na waliwapaka mafuta wagonjwa na wakaponywa.
14 Mfalme Herode aliposikia hayo, kwa kuwa jina la Yesu lilikuwa limejulikana sana. Baadhi walisema, “Yohana mbatizaji amefufuka na kwa sababu hiyo, hii nguvu ya miujiza inafanya kazi ndani yake.”
15 Baadhi yao wakasema, “Huyu ni Eliya,” Bado wengine wakasema, “Huyu ni nabii, kama mmoja wa wale manabii wa zamani.”
16 Lakini Herode aliposikia haya akasema, “Yohana, niliyemkata kichwa amefufuliwa.”
17 Maana Herode mwenyewe aliagiza Yohana akamatwe na alimfunga gerezani kwa sababu ya Herodia (mke wa kaka yake Filipo) kwa sababu yeye alikuwa amemuoa.
18 Kwa maana Yohana alimwambia Herode, “Si halali kumuoa mke wa kaka yako.”
19 Lakini Herodia alianza kumchukia na alikuwa akitaka kumuua, lakini hakuweza,
20 maana Herode alimwogopa Yohana; alijua kwamba ni mwenye haki mtu mtakatifu, na alimwacha salama. Na alipoendelea kumsikiliza alihuzunika sana, lakini alifurahi kumsikiliza.
21 Hata ilipofika wakati mwafaka ikiwa imekaribia siku ya kuzaliwa Herode akawaandalia moafisa wake karamu, na makamanda, na viongozi wa Galilaya.
22 Ndipo binti wa Herodia akaingia na kucheza mbele yao, akamfurahisha Herode na wageni walioketi wakati wa chakula cha jioni. Ndipo mfalme akamwambia binti, “Niombe chochote unachotaka nami nitakupa.”
23 Akamwapia na kusema, chochote utakachoniomba, nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu.”
24 Akatoka nje akamuuliza mama yake, “Niombe nini?” Akasema, “Kichwa cha Yohana Mbatizaji.”
25 Na mara moja akaingia kwa mfalme akaanza kusema, “Nataka unipatie ndani ya sahani, kichwa cha Yohana Mbatizaji.”
26 Mfalme alisikitishwa sana, lakini kwa sababu ya kiapo chake na kwa ajili ya wageni, hakuweza kumkatalia ombi lake.
27 Hivyo, mfalme akatuma askari kati ya walinzi wake na kuwaagiza kwenda kumletea kichwa cha Yohana. Mlinzi alikwenda kumkata kichwa akiwa kifungoni.
28 Akakileta kichwa chake kwenye sahani na kumpatia binti, na binti akampa mama yake.
29 Na wanafunzi wake waliposikia hayo, walikwenda kuuchukua mwili wake wakaenda kuuzika kaburini.
30 Na mitume, walikusanyika pamoja mbele ya Yesu, wakamweleza yote waliyofanya na waliyoyafundisha.
31 Naye akawaambia, “Njooni wenyewe mahali pa faragha na tupumzike kwa muda.” Watu wengi walikuwa wanakuja na kuondoka, hata hawakupata nafasi ya kula.
32 Hivyo wakapanda mashua wakaenda mahali pa faragha peke yao.
33 Lakini waliwaona wakiondoka na wengi wakawatambua, kwa pamoja walikimbia kwa miguu kutoka miji yote, nao wakafika kabla yao.
34 Walipofika pwani, aliona umati mkubwa na akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Na akaanza kuwafundisha mambo mengi.
35 Muda ulipoendelea sana, wanafunzi wakamjia wakamwambia,”Hapa ni mahali pa faragha na muda umeendelea.
36 Uwaage waende miji ya jirani na vijiji ili wakajinunulie chakula.”
37 Lakini akawajibu akisema, “Wapeni ninyi chakula.” Wakamwambia, “Tunaweza kwenda na kununua mikate yenye thamani ya dinari mia mbili na kuwapa wale?”
38 Akawambia,” Mna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.” walipopata wakamwambia, “Mikate mitano na samaki wawili.”
39 Akawaamuru watu waketi katika makundi juu ya majani mabichi.
40 Wakawaketisha katika makundi; makundi ya mamia kwa hamsini.
41 Kisha akachukua mikate mitano na samaki wawili, na kutazama mbinguni, akaibariki kisha akawapa wanafunzi waweke mbele ya umati. Na kisha aligawa samaki wawili kwa watu wote.
42 Walikula wote hadi wakatosheka.
43 Walikusanya vipande vya mikate iliyobaki, Vikajaa vikapu kumi na viwili, na pia vipande vya samaki.
44 Na walikuwa wanaume elfu tano waliokula mikate.
45 Mara akawaambia wapande kwenye mashua waende sehemu nyingine, hadi Bethsaida, wakati Yeye akiwaaga makutano.
46 Walipokuwa wamekwisha kuondoka, akaenda mlimani kuomba.
47 Kulipokuwa jioni, na mashua yao wakati huo ikiwa katikati ya bahari, naye alikuwa peke yake nchi kavu.
48 Na aliwaona wakitaabika kupiga makasia kwa sababu upepo uliwazuia. Ilipokaribia asubuhi akawaendea, akitembea juu ya maji, na alitaka kuwapita.
49 Lakini walipomwona anatembea juu ya maji, wakaingiwa na wasiwasi wakidhani ni mzimu hata wakapiga kelele.
50 kwa sababu walimwona wakajawa na hofu. Mara akasema nao akawaambia, “Muwe wajasiri! ni mimi! Msiwe na hofu.”
51 Akaingia ndani ya mashua, na upepo ukaacha kuvuma, nao wakamshangaa kabisa.
52 Hivyo hawakuwa wameelewa maana ya ile mikate. Maana akili zao zilikuwa na uelewa mdogo.
53 Nao walipovuka ng'ambo, walifika nchi ya Genesareti mashua ikatia nanga.
54 Walipotoka nje ya mashua, mara wakamtambua.
55 Wakakimbia kutangaza katika mkoa mzima na wakaanza kuwaleta wagonjwa kwa machela, kila waliposikia anakuja.
56 Popote alipoingia katika vijiji, au mjini, au katika nchi, waliwaweka wagonjwa mahali pa soko, na wakamsihi awaruhusu kugusa pindo la vazi lake. Na wote waliomgusa waliponywa.