10
1 Yesu akawaita wanafunzi wake kumi na wawili pamoja na kuwapa mamlaka juu ya pepo wachafu, kuwakemea na kuwafukuza na kuponya aina zote za maladhi na aina zote za magonjwa.
2 Majina ya mitume kumi na wawili ni haya. La kwanza simeoni (ambaye pia anaitwa Petro), na Andrea kaka yake, Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana kaka yake:
3 Philipo, na Bartelemayo, Thomaso, na Mathayo mtoza ushuru, Yakobo mwana wa Alfayo, na Tadeo,
4 Simoni mkananayo, na Yuda iskariote, ambaye alimsaliti.
5 Hawa kumi na wawili Yesu aliwatuma. Naye aliwaelekeza akisema “Msiende sehemu wanakoishi wamataifa na msiingie kwenye miji ya wasamalia.
6 Badala yake, mwende kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israel.
7 Na mnapokwenda, hubirini na kusema, ufalme wa mbinguni umekaribia.'
8 Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma na fukuzeni pepo. Mmepokea bure, toeni bure.
9 Msichue dhahabu, almasi au shaba kwenye pochi zenu.
10 Usichukue mkoba katika safari yenu, au nguo za ziada, viatu au fimbo, kwa kuwa mfanyakazi anastahili chakula chake.
11 Mji wowote au kijiji mtakachoingia, tafuteni ambaye anastahili na mkae pale mpaka mtakapoondoka.
12 Mtakapoingia katika nyumba salimieni,
13 endapo nyumba inastahili, amani yenu ibaki pale, lakini kama nyumba haistahili, amani yenu iondoke pamoja nanyi.
14 Na kwa wale wasiowapokea ninyi au kusikiliza maneno yenu, wakati mnaondoka kwenye nyumba au mji huo, jipanguseni mavumbi ya nyayo zenu mahali hapo.
15 Kweli ninawaambia, itakuwa ya kustahimili zaidi miji ya Sodoma na Gomorah siku ya hukumu kuliko mji huo.
16 Angalia, ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu, kwa hiyo iweni na werevu kama nyoka na wapole kama njiwa.
17 Muwe waangalifu na watu, watawapeleka kwenye mabaraza, na watawapiga kwenye masinagogi.
18 Na mtaletwa mbele ya wakuu na wafalme kwa ajili yangu, kama ushuhuda kwao na kwa mataifa.
19 Pindi watakapowashutumu, msiwe na wasiwasi jinsi gani au nini cha kuongea, kwa kuwa kitu cha kusema mtapewa kwa wakati huo.
20 Kwa kuwa sio ninyi mtakaoongea, lakini Roho wa Baba yenu ataongea ndani yenu.
21 Ndugu atamwinukia ndugu yake kumwua, na baba kwa mtoto wake. Watoto watainuka dhidi ya wazazi, na kuwasababishia kifo.
22 Nanyi mtachukiwa na kila mtu kwa sababu ya jina langu. Lakini yeyote atakayevumilia mpaka mwisho mtu huyo ataokolewa.
23 Pindi wanapowatesa katika mji huu, kimbilieni mji unaofuata, kwa kweli ninawaambia, hamtakuwa mmekwenda kwenye miji yote ya Israeli kabla ya mwana wa Adam hajarudi.
24 Mwanafunzi si mkuu kuliko mwalimu wake, wala mtumwa aliye juu ya Bwana wake.
25 Inatosha kwa mwanafunzi kwamba awe kama mwalimu wake, na mtumishi kama Bwana wake. Ikiwa wamemwita Bwana wa nyumba Belzabuli, ni kwa kiasi gani zaidi watawakashifu wa nyumba yake!
26 Hivyo basi msiwahofu wao, kwa kuwa hakuna jambo ambalo halitafunuliwa, na hakuna lililofichika ambalo halitajulikana.
27 Kile ninachowaambia gizani, mkiseme nuruni, na mnachokisikia kwa ulaini masikioni mwenu, mkitangaze mkiwa juu ya nyumba.
28 Msiwaogope wale ambao wanaua mwili lakini hawana uwezo wa kuua roho. Badala yake, mwogopeni yule ambaye awezaye kuangamiza mwili na roho kule kuzimu.
29 Je kasuku wawili hawauzwi kwa senti ndogo? Hata hivyo hakuna anayeweza kuanguka chini bila Baba yenu kufahamu.
30 Lakini hata idadi ya nywele zenu zimehesabiwa.
31 Msiwe na hofu, kwa kuwa mnathamani zaidi kuliko kasuku wengi.
32 Hivyo basi kila mmoja atakaye nikiri mbele za watu, nami pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.
33 Lakini yeye atakaye nikana mbele za watu, nami pia nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.
34 Msifikiri kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani, lakini upanga.
35 Kwa kuwa nilikuja kumweka mtu apingane na baba yake, na binti dhidi ya mama yake, na mkwe dhidi ya mama mkwe wake.
36 Adui wa mtu watakuwa wale wa nyumbani mwake.
37 Yeye ambaye anampenda baba au mama zaidi kuliko mimi huyo hanistahili. Na yeye anayempenda kijana au binti zaidi kuliko mimi huyo hanistahili.
38 Yeye ambaye hatabeba msalaba na kunifuata mimi hanistahili.
39 Yeye atakayetafuta maisha atayapoteza. Lakini yeye atakayepoteza maisha kwa ajili yangu atayapata.
40 Yeye atakayewakaribisha amenikaribisha mimi, na yeye atakayenikaribisha mimi amemkaribisha yeye aliyenituma mimi.
41 Na yeye atakayemkaribisha nabii kwa sababu ni nabii atapokea thawabu ya nabii. Na yeye atakayemkaribisha mwenye haki kwa sababu ni mtu wa haki atapokea thawabu ya mtu wa haki.
42 Yeyote atakayempatia mmoja wa wadogo hawa, hata kikombe cha maji ya kunywa ya baridi, kwa sababu yeye ni mwanafunzi, kweli ninawaambia, yeye hawezi kukosa kwa njia yeyote thawabu yake.”