8
1 Wakati Yesu aliposhuka chini kutoka mlimani, umati mkubwa ulimfuata.
2 Tazama, mkoma alikuja na kusujudu mbele yake, akasema, “Bwana, ikiwa uko tayari, unaweza kunifanya niwe safi”.
3 Yesu akanyoosha mkono wake na kumgusa, akasema, “Niko tayari. Uwe msafi.” Hapo hapo alitakaswa ukoma wake.
4 Yesu akamwambia, “Angalia kwamba usiseme kwa mtu yeyote. Shika njia yako, na jioneshe mwenyewe kwa kuhani na utoe zawadi ambayo Musa aliagiza, kwa ajili ya ushuhuda kwao”
5 Wakati Yesu alipofika Kapernaumu, Jemedari akaja kwake akamuuliza
6 akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani amepooza na ana maumivu ya kutisha.”
7 Yesu akamwambia, “Nitakuja na kumponya”.
8 Jemedari akajibu na kumwambia, “Bwana, mimi si wathamani hata uje na kuingia ndani ya dari yangu, sema neno tu na mtumishi wangu ataponywa.
9 Kwa kuwa mimi pia ni mtu niliye na mamlaka, na ninao askari walio chini yangu. Nikisema kwa huyu “Nenda' na huenda, na kwa mwingine 'Njoo' na yeye huja, na kwa mtumishi wangu, 'Fanya hivi,' na yeye anafanya hivyo”
10 Wakati Yesu aliposikia haya, alishangazwa na kuwaambia wale waliokuwa wakimfuata, “Kweli ninawaambia, Sijapata kuona mtu mwenye imani kama huyu katika Israel.
11 Ninawambieni, wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, wataketi katika meza pamoja na Abrahimu, Isaka, na Yakobo, katika ufame wa mbinguni.
12 Lakini watoto wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ambapo kutakuwa na kilio na kusaga meno.”
13 Yesu akamwambia Jemadari, “Nenda! Kama ulivyokwisha amini, na itendeke hivyo kwako”. Na mtumishi aliponywa katika saa hiyo.
14 Wakati Yesu alipofika kwenye nyumba ya Petro, alimwona mama mkwe wake na Petro amelala akiwa mgonjwa wa homa.
15 Yesu akamgusa mkono wake, na homa yake ikamwacha. kisha akaamka akaanza kumhudumia.
16 Na ilipofika jioni, watu wakamletea Yesu wengi waliotawaliwa na pepo. Akawafukuza pepo na wale walio wagonjwa akawaponya.
17 Kwa jinsi hii yalitimia yale yaliyo kwisha kunenwa na Isaya nabii, “Yeye mwenyewe alichukua magonjwa yetu na alibeba maradhi yetu”
18 Kisha Yesu alipoliona kusanyiko limemzunguka, alitoa maelekezo ya kwenda upande mwingine wa Bahari ya Galilaya.
19 Kisha mwandishi akaja kwake na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata popote utakapoenda.”
20 Yesu akamwambia, “Mbweha wana mashimo, na ndege wa angani wana viota, lakini mwana wa Adamu hana sehemu ya kulaza kichwa chake.”
21 Mwanafunzi mwingine akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza niende kumzika baba yangu.”
22 Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate, na uwaache wafu wazike wafu wao.”
23 Yesu alipoingia kwenye mtumbwi, wanafunzi wake wakamfuata mtumbwini.
24 Tazama, ikainuka dhoruba kuu juu ya bahari, kiasi kwamba mtumbwi ulifunikwa na mawimbi. Lakini Yesu alikuwa amelala.
25 Wanafunzi wakaja kwake na kumwamsha wakisema, “Bwana, tuokoe sisi, tunaelekea kufa!”
26 Yesu akawaambia, “kwa nini mnaogopa, ninyi wenye imani ndogo?” Ndipo akaamka na kuukemea upepo na bahari. Kisha kukawa na utulivu mkuu,
27 wanaume wakashikwa na mshangao wakasema, “Huyu mtu niwa namna gani, kwamba hata pepo na bahari vinamtii yeye?”
28 Wakati Yesu alipokuwa amekuja upande mwingine wa nchi ya Magadala, wanaume wawili waliotawaliwa na pepo walikutana naye. Walikuwa wakitokea makaburini na walikuwa wakifanya vurugu sana, kiasi kwamba hakuna msafiri angeweza kupita njia ile.
29 Tazama, walipaza sauti na kusema, “Tuna nini cha kufanya kwako, mwana wa Mungu? Umekuja hapa kututesa kabla ya wakati kufika?”
30 Sasa kundi kubwa la nguruwe lilikuwa likichunga, hapakuwa mbali sana walipokuwa,
31 pepo waliendelea kulalamika kwa Yesu na kusema. “Ikiwa utatuamuru kutoka, tupeleke kwenye kundi la nguruwe.”
32 Yesu akawaambia, “Nendeni!” Pepo wakawatoka na kwenda kwa nguruwe. Na tazama, kundi lote likashuka kutoka mlimani kuteremkia baharini na lote likafia majini.
33 Wanaume waliokuwa wakichunga nguruwe walikimbia. Na walipoenda mjini wakaelezea kila kitu, hususani kilichotokea kwa wanaume waliotawaliwa na mapepo.
34 Tazama, mji mzima ukaja kukutana na Yesu. Walipomwona, walimsihi aondoke kwenye mkoa wao.