16
1 Mipango ya moyo ni ya mtu, bali Yehova hutoa jawabu kutoka kwenye ulimi wake.
2 Njia zote za mtu ni safi kwenye macho yake mwenyewe, bali Yehova huipima mioyo.
3 Kabidhi kwa Yehova kazi zako zote na mipango yako itafanikiwa.
4 Yehova alifanya kila kitu kwa kusudi lake, hata waovu kwa ajili ya siku ya taabu.
5 Yehova anamchukia kila mtu mwenye moyo wa majivuno, ingawa wanasimama imara, hawakosi kupata adhabu.
6 Kwa agano la uaminifu na udhamini uovu husafishwa na kwa kumcha Yehova watu hujitenga na ubaya.
7 Njia za mtu zinapompendeza Yehova, huwafanya hata adui zake huyo mtu wawe na amani naye.
8 Bora kitu kidogo pamoja na haki, kuliko mapato makubwa pamoja na udhalimu.
9 Katika moyo wake mtu hunuia njia yake, bali Yehova huziongoza hatua zake.
10 Mshauri yupo katika midimo ya mfalme, katika hukumu kinywa chake hakisemi kwa udanganyifu.
11 Vipimo vya kweli hutoka kwa Yehova; uzito wote kwenye gunia ni kazi yake.
12 Wafalme wanapofanya mambo maovu, hicho ni kitu cha kudharauliwa, kwa maana utawala huimarishwa kwa kutenda haki.
13 Mfalme hufurahia midomo ambayo husema haki na anampenda mwenye kusema waziwazi.
14 Hasira ya mfalme ni mjumbe wa mauti lakini mtu mwenye busara atajaribu kutuliza hasira yake.
15 Katika nuru ya uso wa mfalme ni uzima na fadhila yake ni kama wingu linaloleta mvua ya masika.
16 Ni bora kiasi gani kupata hekima kuliko dhahabu. Kuchagua kupata ufahamu ni zaidi kuliko fedha.
17 Njia kuu ya watu waadilifu hujitenga na ubaya; mwenye kuyahifadhi maisha yake huilinda njia yake.
18 Kiburi hutangulia kabla ya uharibifu na moyo wa kujivuna kabla ya maangamizi.
19 Ni bora kunyenyekea miongoni mwa watu masikini kuliko kugawana ngawira pamoja watu wenye kiburi.
20 Mwenye kutafakari yaliyofundishwa hupata kilicho chema na wenye kumtumaini Yehova watafurahi.
21 Mwenye hekima moyoni anaitwa ufuhamu na utamu wa hotuba huongeza uwezo wa kufundisha.
22 Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwake ambaye nayo, bali adhabu ya wapumbavu ni upumbavu wao.
23 Moyo wa mtu mwenye hekima hutoa busara katika kinywa chake na huongeza ushawishi katika midomo yake.
24 Maneno yenye kufaa ni sega la asali -matamu kwenye nafsi na huponya mifupa.
25 Kuna njia ambayo huonekana sawa kwa mtu, bali mwisho wake ni njia ya mauti.
26 Hamu ya kibarua humfanyia kazi; njaa yake humsihi kuendelea.
27 Mtu duni huchimba madhara na usemi wake ni kama moto unaounguza.
28 Mtu mkaidi huchochea mafarakano na umbeya huwafarakanisha marafiki.
29 Mtu wa vurugu humdanganya jirani yake na kumwongoza kwenye mapito ambayo si mema.
30 Yule anayekonyeza kwa jicho anapanga njama za mambo ya ukaidi; wenye kuandama midomo yao watapitisha mabaya.
31 Mvi ni taji ya utukufu; hupatikana kwa kuishi katika njia ya haki.
32 Ni bora kukawia kuwa na hasira kuliko kuwa shujaa na mwenye kutawala roho yake ni imara zaidi kuliko yule anayeuteka mji.
33 Kura hurushwa kwenye mkunjo, bali maamuzi hutoka kwa Yehova.