Zaburi
1
1 Amebarikiwa mtu yule asiye enenda katika ushauri wa waovu, au kusimama katika njia ya wenye dhambi, au kukaa katika kusanyiko la wenye mizaha.
2 Bali yeye huifurahia sheria ya Yahwe, na huitafakari sheria yake mchana na usiku.
3 Atakuwa kama mti uliopandwa karibu na mkondo wa maji ambao huzaa matunda yake kwa majira yake, ambao majani yake hayakauki; lolote afanyalo litafanikiwa.
4 Waovu hawako hivyo, wao badala yake ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
5 Kwa hivyo waovu hawatasimama katika hukumu, wala wenye dhambi katika kusanyiko la wenye haki.
6 Kwa kuwa Yahweh huikubali njia ya wenye haki, njia ya waovu itaangamizwa.