107
1 Mshukuruni Yahwe, maana ni mwema, na uaminifu wa agano lake wadumu milele.
2 Waseme hivi waliokombolewa na Yahwe, wale aliowaokoa toka mkononi mwa adui.
3 Yeye amewakusanya kutoka nchi za kigeni, kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini.
4 Walitanga-tanga janwani katika njia ya nyika hawakuona mji wa kuishi.
5 Kwa sababu walikuwa na njaa na kiu, walikata tamaa kutokana na uchovu.
6 Kisha walimuita Yahwe katika shida yao, naye aliwaokoa toka katika dhiki yao.
7 Aliwaongoza kupitia njia ya moja kwa moja waweze kwenda mjini kuishi humo.
8 Oh ili watu wamsifu Yahwe kwa ajili ya uaminifu wa agano lake na kwa mambo ya ajabu aliowatendea wanadamu!
9 Maana hutosheleza shauku za walio na kiu, na hamu ya wale wenye njaa yeye huwashibisha kwa mambo mema.
10 Baadhi walikaa katika giza na uvuli wa mauti, walifungwa katika mateso na minyororo.
11 Hii ni kwa sababu walikuwa wameliasi neno la Mungu na walikataa maelekezo ya Aliye Juu.
12 Aliinyenyekesha mioyo yao kupitia magumu; walipata mashaka na hakukuwa na mmoja wa kuwasaidia.
13 Kisha wakamwita Yahwe katika shida yao, naye akawatoa katika dhiki yao.
14 Aliwatoa gizani na kwenye uvuli wa mauti na kuvunja vifungo vyao.
15 Oh ili watu wamsifu Yahwe kwa ajili ya uaminifu wa agano lake na kwa mambo ya ajabu aliyoyatenda kwa wanadamu!
16 Kwa maana amevunja malango ya shaba na kukata mapingo ya chuma.
17 Walikuwa wapumbavu katika njia zao za uasi na kuteswa kwa sababu ya dhambi zao.
18 Walipoteza hamu yao ya kula chakula chochote, na waliyakaribia malango ya kifo.
19 Kisha walimlilia Yahwe katika shida yao, naye akawatoa katika dhiki yao.
20 Alituma neno lake na likawaponya, na akawaokoa kutoka katika uharibifu wao.
21 Oh ili watu wamsifu Yahwe kwa ajili ya uaminifu wa agano lake na kwa mambo ya ajabu aliyoyatenda kwa wanadamu!
22 Na watoe dhabihu ya shukrani na kutangaza matendo yake kwa kuimba.
23 Baadhi husafiri baharini katika meli na kufanya biashara juu ya bahari.
24 Hawa huona matendo ya Yahwe na maajabu yake baharini.
25 Kwa maana aliamuru na alivumisha upepo wa dhoruba ambao uliyainua juu mawimbi ya baharini.
26 Walipanda juu mawinguni na kushuka vilindini. Nafsi zao ziliyeyuka katika dhiki.
27 Waliyumba-yumba na kupepesuka kama walevi na hawakujua la kufanya.
28 Kisha walimlilia Yahwe katika shida yao, naye akawatoa katika dhiki yao.
29 Aliituliza dhoruba, na mawimbi yakatulia.
30 Ndipo walifurahia kwa sababu bahari ilikuwa shwali, na aliwaleta kwenye bandari waliyoitamani.
31 Oh, ili watu wamsifu Yahwe kwa ajili ya uaminifu wa agano lake na kwa mambo ya ajabu aliyowatendea wanadamu!
32 Wamtukuze yeye katika kusanyiko la watu na wamsifu yeye katika baraza la viongozi.
33 Aligeuza mito ikwa jangwa, chemchem ya maji ikawa nchi kame,
34 na nchi ya matunda mengi ikawa nchi isiyozaa kwa sababu ya uovu wa watu wake.
35 Aligeuza jangwa likawa ziwa la maji na nchi kame ikawa chemchem ya maji.
36 Aliwakalisha huko wenye njaa, nao walijenga mji na kuishi humo.
37 Walijenga mji ili kupanda mimea shambani, kupanda mizabibu, na kuleta humo mazao tele.
38 Yeye huwabariki wameongezeka sana katika hesabu. Haachi mifugo yao ipungue katika hesabu.
39 Kisha wakapungua na kudhilika kwa dhiki na mateso.
40 Akawamwagia viongozi dharau na akawafanya wazunguke katika jangwa, mahali pasipo na njia.
41 Lakini aliwalinda wahitaji dhidi ya mateso na kujali kwa ajili ya familia yake kama kundi la kondoo.
42 Wenye haki wataona hili na kufurahi, na uovu wote utaona na kufunga kinya chake.
43 Yeyote mwenye hekima anapaswa kuyaangalia haya na kutafakari juu ya matendo ya uaminifu wa agano la Yahwe.