132
Wimbo wa kwenda hekaluni kuabudu.
1 Yahwe, kwa ajili ya Daudi kumbuka mateso yake yote.
2 Kumbuka ndiye aliye mwapia Yahwe, aliweka nadhiri kwa Shujaa wa Yakobo.
3 Alisema, sitaingia nyumbani mwangu wala sitaenda kitandani mwangu,
4 sitayapa macho yangu usingizi wala kope zangu kupumzika
5 mpaka nitakapopata mahali kwa ajili ya Yahwe, na maskani kwa ajili ya Shujaa wa Yakobo.”
6 Tazama tulisikia kuhusu hilo katika Efrata; tuliipata katika konde la Yearimu.
7 Tutaingia katika maskani ya Mungu; tutasujudu miguuni pake.
8 Inuka, Ee Yahwe, uje mahali pako pa kupumzika, wewe na sanduku la nguvu zako!
9 Makuhani wako na wavikwe uadilifu; waaminifu wako washangilie.
10 Kwa ajili ya mtumishi wako Daudi, usimuache mfalme wako uliye mpaka mafuta.
11 Yahwe alimwapia Daudi kiapo cha uhakika, kiapo cha uhakika ambacho hatakivunja: “Nitamuweka mmoja wa wazawa wako kwenye kiti chako cha enzi.
12 Kama wana wako watalishika agano langu na sheria ambazo nitawafundisha, watoto wao pia watakaa kwenye kiti chako cha enzi milele.”
13 Hakika Yahwe ameichagua Sayuni, ameitamani kwa ajili ya makao yake.
14 “Hapa ni mahali pangu pa kupumzika milele. Nitaishi hapa, kwa kuwa ninapatamani.
15 Nitapabariki sana kwa mahitaji. Nitawatosheleza maskini wake kwa mkate.
16 Nitawavisha makuhani wake kwa wokovu, waaminifu wake watashangilia kwa furaha.
17 Hapo nitachipusha pembe kwa ajili ya Daudi na kuweka taa juu kwa ajili ya mpakwa mafuta wangu.
18 Nitawavisha adui kwa aibu, bali juu yake taji yake itang'aa.”