142
Zaburi ya Daudi, alipokuwa pangoni; maombi.
1 Kwa sauti yangu namlilia Yahwe anisaidie; kwa sauti yangu naomba kwa ajili ya neema ya Yahwe.
2 Namwaga malalamiko yangu mbele zake; ninamwambia shida zangu.
3 Roho yangu inapokuwa dhaifu ndani yangu, wewe unajua mapito yangu. Kwenye njia niipitayo wamenifichia mtego.
4 Natazama kulia kwangu na sioni yeyote anayenijali. Sina pa kukimbilia; hakuna anayejali kuhusu uhai wangu.
5 Nilikuita wewe, Yahwe; nikasema, “Wewe ni kimbilio langu, fungu langu katika nchi ya walio hai.
6 Sikia kuita kwangu, maana nimeshushwa chini sana; uniokoe dhidi ya watesi wangu, maana wana nguvu kuliko mimi.
7 Uitoe nafsi yangu kifungoni ili niweze kulishukuru jina lako. Wenye haki watakusanyika karibu nami kwa sababu umekuwa mwema kwangu.”