143
Zaburi ya Daudi.
1 Ee Yahwe, usikie maombi yangu; sikia kuomba kwangu. Kwa sababu ya uaminifu wa agano lako na haki yako, unijibu!
2 Usimuhukumu mtumishi wako, kwa kuwa machoni pako hamna aliye haki.
3 Adui ameifuatia nafsi yangu; amenisukuma hadi chini; amenifanya niishi gizani kama wale ambao wamekwisha kufa siku nyingi zilizopita.
4 Na roho yangu inazidiwa ndani yangu; moyo wangu unakata tamaa.
5 Nakumbuka siku za zamani zilizopita; nayatafakari matendo yako yote; nawaza juu ya utimilifu wako.
6 Nakunyoshea mikono yangu katika maombi; nafsi yangu inakuonea kiu katika nchi kavu. Selah
7 Unijibu upesi, Yahwe, kwa sababu roho yangu inazimia. Usinifiche uso wako, vinginevyo nitakuwa kama wale waendao chini shimoni.
8 Unifanye kusikia uaminifu wa agano lako wakati wa asubuhi, maana ninakuamini wewe. Unionyeshe njia niipasayo kutembea kwayo, kwa maana nakuinulia wewe nafsi yangu.
9 Uniokoe dhidi ya adui zangu, Yahwe; nakimbilia kwako ili nijifiche.
10 Unifundishe kufanya mapenzi yako, maana wewe ni Mungu wangu. Roho wako mwema na aniongoze mimi katika nchi ya unyoofu.
11 Ee Yahwe, kwa ajili ya jina lako, unihifadhi hai; katika haki yako uitoe nafsi yangu taabuni.
12 Katika uaminifu wa agano lako uwaondoshe maadui zangu na uwaangamize maadui wa uhai wangu, maana mimi ni mtumishi wako.