27
Zaburi ya Daudi.
1 Yahwe ni nuru yangu na wokovu wangu; nimuogope nani? Yahwe ni salama ya maisha yangu; ni mhofu nani?
2 Wakati waovu waliponijia kunila mwili wangu, wapinzani wangu na adui zangu walijikwaa na wakaanguka.
3 Ingawa jeshi hujipanga kupigana na mimi, moyo wangu hautaogopa; japo vita vijapo inuka kupigana nami hata hapo nitabaki kuwa jasiri.
4 Kitu kimoja nimekiomba kwa Yahwe, nami nitakitafuta hicho: kwamba niweze kukaa katika nyumba ya Yahwe siku zote za maisha yangu, kuutazama uzuri wa Yahwe na kutafakari hekaruni mwake.
5 Kwa kuwa katika siku ya shida atanificha nyumbani mwake; atanificha katika mfuniko wa hema lake. Yeye ataniinua juu ya mwamba!
6 Kisha kichwa changu kitainuliwa juu ya maadui wote wanizungukao, nami nitatoa sadaka ya furaha hemani mwake! Nitaimba na kutunga nyimbo kwa Yahwe!
7 Sikia, sauti yangu nikuitapo, Yahwe! Unihurumie, na unijibu!
8 Moyo wangu huongea kuhusu wewe, “Utafute uso wake!” Nami nautafuta uso wako, Yahwe!
9 Usiufiche uso wako mbali na mimi; usinikasirikie mimi mtumishi wako! Wewe umekuwa msaada wangu; usiniache wala kunitelekeza, Mungu wa wokovu wangu!
10 Hata kama baba yangu na mama yangu wakiniacha, Yahwe utanitunza kwako.
11 Unifundishe njia yako, Yahwe! Kwa sababu ya adui zangu uniongoze katika njia salama.
12 Usiwaache adui zangu wanifanyie watamanivyo, kwa sababu mashahidi wa uongo wameinuka kinyume namimi, nao wanapumua vurugu!
13 Kitu gani kingeweza kunitokea kama nisingeamini kuwa nitauona uzuri wa Yahwe katika nchi ya walio hai?
14 Umngoje Yahwe; uwe imara, na moyo wako uwe jasiri! Umngoje Yahwe!