30
Zaburi; wimbo wakati wa kuweka wakifu hekalu. Zaburi ya Daudi.
1 Nitakutukuza wewe, Yahwe, kwa kuwa umeniinua na haujawaruhusu maadui zangu juu yangu.
2 Yahwe Mungu wangu, nilikulilia wewe kwa ajili ya msaada, nawe ukaniponya.
3 Yahwe, wewe umeitoa roho yangu kuzimuni; nawe umeniweka hai mbali na kaburi.
4 Mwimbieni sifa Yahwe, ninyi waaminifu wake! Mshukuruni Bwana mkumbukapo utakatifu wake.
5 Kwa kuwa hasira yake ni ya muda tu; bali neema yake yadumu milele. Kilio huja usiku, bali furaha huja asubuhi.
6 Kwa ujasiri nilisema, “Sitatikiswa kamwe.”
7 Yahwe, kwa neema yako uliniweka mimi kama mlima imara; lakini ulipouficha uso wako, nilisumbuka.
8 Nilikulilia wewe, Yahwe, na kuomba msaada kwa Bwana wangu!
9 Kuna faida gani katika kifo changu, kama nitaenda kaburini? Je, mavumbi yatakusifu wewe? Yatatangaza uaminifu wako?
10 Sikia, Yahwe, na unihurumie! Yahwe, uwe msaidizi wangu.
11 Wewe umegeuza kuomboleza kwangu kuwa kucheza; wewe umeyaondoa mavazi yangu ya magunia na kunivisha furaha.
12 Hivyo sasa utukufu wangu utakuimbia sifa wewe na hautanyamaza; Yahwe Mungu wangu, nitakushukuru wewe milele!