29
Zaburi ya Daudi.
1 Mpeni sifa Yahwe, enyi wana wa Mungu! Mpeni sifa Yahwe kwa ajili ya utukufu wake na nguvu.
2 Mpeni Yahwe utukufu ambao jina lake linastahili. Mpigieni magoti Yahwe katika mapambo ya utakatifu.
3 Sauti ya Yahwe imesikika zaidi ya maji; Mungu wa radi ya utukufu, radi yaYahwe i juu ya maji mengi.
4 Sauti ya Yahwe ina nguvu; sauti ya Yahwe ni kuu.
5 Sauti ya Yahwe huivunja mierezi; Yahwe huivunja vipande vipande mierezi ya Lebanon.
6 Yeye huifanya Lebanoni kuruka kama ndama wa ng'ombe na Sirioni kama mwana wa nyati.
7 Sauti ya Yahwe hutoa miale ya moto.
8 Sauti ya Yahwe hutetemesha Jangwa; Yahwe hutetemesha jangwa la Kadeshi.
9 Sauti ya Yahwe huufanya miti mikubwa kutikisika na huipukutisha misitu. Kila mmoja katika hekalu lake husema, “Utukufu!”
10 Yahwe hukaa kama mfalme juu ya mafuriko; Yahwe hukaa kama mfalme milele.
11 Yahwe huwatia nguvu watu wake; Yahwe huwa bariki watu wake na amani.