40
Kwa kiongozi wa muziki. Zaburi ya Daudi.
1 Nalimungoja Yahwe kwa uvumilivu; alinisikia na kusika kilio changu.
2 Yeye akanitoa nje ya shimo la kutisha, nje ya matope, naye aliiweka miguu yangu juu ya mwamba na kuzifanya hatua zangu salama.
3 Yeye ameweka wimbo mpya mdomoni mwangu, sifa kwa Mungu. Wengi watauona na kumheshimu yeye na kumwamini Yahwe.
4 Amebarikiwa mtu yule ambaye humfanya Yahwe tumaini lake naye hathamini majivuno wala wale wanaokengeuka kwa uongo.
5 Yahwe Mungu wangu, matendo ya ajabu ambayo wewe umeyafanya, ni mengi, na mawazo yako yatuhusuyo sisi hayahesabiki; Ikiwa ningetangaza na kuyazungumza kwao, ni mengi sana hayahesabiki.
6 Wewe haufurahishwi katika sadaka au matoleo, bali wewe umeyafungua masikio yangu; wala haukuhitaji sadaka ya kuteketeza au sadaka ya dhambi.
7 Ndipo nilisema mimi, “Tazama, nimekuja; imeandikwa kuhusu mimi katika kitabu cha hati.
8 Ninafurahia kuyafanya mapenzi yako, Mungu wangu; sheria zako ziko moyoni mwangu.”
9 Katika kusanyiko kubwa nimetangaza habari njema ya haki yako; Yahwe, wewe unajua sikuizuia midomo yangu.
10 Sikuficha haki yako moyoni mwangu; nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako; sijaficha uaminifu wa agano lako au uaminifu wako kwenye kusanyiko kubwa.
11 Usiache kunitendea kwa rehema, Yahwe; Uaminifu wa agano lako na uaminifu wako unihifadhi siku zote.
12 Mabaya yasiyo hesabika yamenizunguka; Maovu yangu yamenipata nami siwezi kuona chochote; nayo ni mengi kuliko nywele za kichwa changu, na moyo wangu umeniangusha.
13 Yahwe, tafadhari uniokoe; njoo haraka unisaidie Yahwe.
14 Waaibike na wafedheheke kabisa wanaufuatilia uhai wangu wauondoe. Warudishwe nyuma na wadharaulike, wale wanaofurahia kuniumiza.
15 Waogopeshwe kwa sababu ya aibu yao, wale waniambiao, “Aha, aha!”
16 Bali wale wote wakutafutao wafurahi na kushangilia katika wewe; na kila mmoja apendaye wokovu wako aseme daima, “Asifiwe Yahwe.”
17 Mimi ni maskini na muhitaji; lakini Bwana hunifikiria. Wewe ni msaada wangu nawe huja kuniokoa; usichelewe, Mungu wangu.