42
Kwa kiongozi wa muziki. Zaburi ya wana wa Korah
1 Kama ayala ayatamanivyo maji ya mto. ndivyo hivyo ninakiu yako, Mungu.
2 Ninakiu yako Mungu, Mungu uliye hai, ni lini nitaonekana mbele zako?
3 Machozi yangu yamekuwa ni chakula changu mchana na usiku, wakati maadui zangu siku zote wanasema, “Yuko wapi Mungu wako?”
4 Mambo haya niayakumbuka ninapoumimina roho yangu: nilipoenda na umati wa watu na kuwaongoza kwenye nyumba ya Mungu kwa sauti ya shangwe na kusifu, ni wengi tulisherekea.
5 Roho yangu, kwa nini unainama? Kwa nini unahuzuni ndani yangu? Mtumaini Mungu, Kwa kuwa kwa mara nyingine nitamsifu yeye ambaye ni wokovu wangu.
6 Mungu wangu, roho yangu imeinama ndani yangu, kwa hiyo ninakukumbuka toka nchi ya Yordani, toka kwenye vilele vitatu vya mlima Hermoni, na toka mlima wa Mizari.
7 Kina huita kina kwenye kelele za maporomoko ya maji yako; mawimbi na mafuriko yako yote yako juu yangu.
8 Wakati wa mchana Yahwe ataamuru uaminifu wa agano lake; na usiku wimbo wake utakuwa nami, ombi kwa Mungu wa uhai wangu.
9 Nami nitasema kwa Mungu wangu, mwamba wangu, “Kwa nini umenisahau? Kwa nini ninaenenda katika maombolezo kwa sababu ya ukandamizaji wa adui yangu?”
10 Kama upanga mifupani pangu, maadui zangu wananikemea, siku zote wakiniambia, “Yuko wapi Mungu wako?”
11 Roho yangu, kwa nini umeinama chini? Kwa nini unahuzuni ndani yangu? Mtumaini Mungu kwa kuwa nitamsifu tena yeye aliye wokovu wangu na Mungu wangu.